• HABARI MPYA

    Tuesday, September 25, 2012

    YANGA WAKWAMA KUINGIA KAMBINI, SIMBA TAYARI WAPO MBWENI

    Yanga SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA ya Dar es Salaam, imekwama kuingia kambini leo Bagamoyo mkoani Pwani, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC , Oktoba 3, mwaka huu na sasa zoezi hilo litafanyika kesho.
    Wakati Yanga, wakishindwa kuingia kambini leo, wapinzani wao wa jadi, Simba SC, tayari wapo maeneo ya Mbweni, visiwani Zainzbar tangu saa 11:00 jioni wakijiandaa na mchezo huo wa kukata na shoka, ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport.
    Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba timu hiyo itaingia kesho na itarudi Dar es Salaam Septemba 30, kucheza na African Lyon, na baada ya mechi itarejea huko kuendelea kujiandaa na pambano la watani.
    Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua, kwa sababu mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Yanga ilifungwa mabao 5-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kipigo hicho ilidaiwa kilitokana na uongozi dhaifu chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na pia ilikuwa sababu ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo na kufanyika uchaguzi mdogo, uliomuweka madarakani Yussuf Manji, Mwenyekiti mpya.
    Tangu wakati wa kampeni, miongoni mwa mambo ambayo wana Yanga wamekuwa wakiomba kutoka kwa Manji ni kulipiwa kisasi cha 5-0, ingawa kwa hali ya sasa ya timu hizo, ubora wao haupishani sana, hakuna hakika kama hilo litawezekana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAKWAMA KUINGIA KAMBINI, SIMBA TAYARI WAPO MBWENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top