• HABARI MPYA

    Saturday, September 29, 2012

    SIMBA SC BILA BOBAN, OKWI KUREJEA KILELENI LIGI KUU LEO?

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC inashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Prisons ya Mbeya katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mchezo ambao utaanza saa 1:00 usiku na kuonyeshwa moja kwa moja Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini.
    Huo utakuwa mchezo wao wa mwisho kabla ya kushuka dimbani Jumatano kumenyana na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC katika mfululizo wa ligi hiyo.
    Aidha, Simba SC itahitaji ushindi katika mchezo wa leo, ili kurejea kileleni, kufuatia Azam FC jana kuitandika JKT Ruvu 3-0 kupaa kileleni, sasa ikiwazidi Wekundu wa Msimbazi pointi moja.
    Lakini mbele ya Prisons, kwa wenye kukumbuka historia ya mechi baina ya timu hizo, kabla haijashuka Daraja, kama imerejea na makali yale yale, mchezo wa leo utakuwa mgumu.   
    Katika mchezo wa leo, kocha Mserbia wa Simba, Milovan Cirkovick anatarajiwa kuwakosa wakali wake wawili, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye ni mgonjwa na Emmanuel Okwi, anayetumikia adhabu.
    Boban aliingia dakika za mwishoni kwenye mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Ruvu Shooting, kwa sababu alikuwa anaumwa na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa alikuwa anajisikilizia afya yake.
    Kuna uwezekano mkubwa Boban akapanda boti na wenzake na baada ya mechi ya leo, dhidi ya Prisons.
    Japo Boban hakuwa kambini Zanzibar, lakini Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
    Morali ya kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3, kuanzia sa 1:00 usiku.
    Simba inarejea leo Dar es Salaam kucheza mechi na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, na baada ya mchezo huo itarejea tena visiwani humo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumamosi ijayo.
    Hata hivyo, katika mechi ya Yanga pia, Simba itamkosa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi ambaye amefungiwa na Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya Mwenyekiti wake, Wallace Karia, sambamba na kumtoza faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.
    Okwi alifanya hivyo akilipa kisasi cha kuchezewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tayari Okwi amekosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, na sasa atakosa mechi mbili zaidi, dhidi ya Prisons na dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru kuendelea kumtumikia mwajiri wake.
    Siyo siri, kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi alikuwa ni homa kwa Yanga, hasa wakikumbuka namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC BILA BOBAN, OKWI KUREJEA KILELENI LIGI KUU LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top