• HABARI MPYA

    Saturday, September 29, 2012

    SIMBA WATUMA SALAMU YANGA, WAWAPIGA MAAFANDE WA PRISONS TAIFA

    Ngassa
    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC leo imeendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.
    Kwa ushindi huo, imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa, nne.
    Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zikwishafungana bao 1-1, Prisons wakitangulia kupata bao dakika ya sita baada ya Maguri kuwatoka mabeki wa Simba kupiga shuti lililomgonga Shomary Kapombe na kumchanganya kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja na kutinga nyavuni.
    Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Prisons waliendelea kuwa wagumu, hadi walipojisahau kidogo sekunde za mwishoni za kipindi cha kwanza na Felix Sunzu akatumia pasi ya Amiri Maftah kusawazisha dakika ya 45.
    Kipindi cha pili, Simba walirudi na moto na kuanza moja kwa moja kulishambulia mfululizo lango la Prisons na dakika ya 55 Ngassa akafunga kwa shuti dhaifu, ambalo kipa wa Prisons, David Abdallah alidaka lakini mpira ukamtoka na kuingia nyavuni.
    Mechi hiyo ilichezeshwa na refa, Paul Soleji kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo, mshika kibendera namba moja, Mwarabu Mumba mshika kibendera namba mbili, wote kutoka Morogoro, wakati refa wa Akiba alikuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam. 
    Dakika ya 87 Amir Maftah alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Khalid Fupi wa Prisons, hivyo ataukosa mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumatano na hiyo ni nafasi kwa chipukizi Paul Ngalema.
    Hiyo inakuwa kadi ya pili nyekundu kwa Simba ndani ya mechi nne, awali katika mechi ya pili dhidi ya JKT Ruvu, Emmanuel Okwi alilimwa kadi ya aina hiyo kwa kumpiga kiwiko Kessy Mapande na akafungiwa mechi tatu.
    Simba sasa inarejea kambini kwake visiwani Zanzibar kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumatano, wakati watani wao, Yanga walioweka kambi Changanyikeni, Dar es Salaam kesho watacheza na African Lyon Uwanja wa Taifa.
    Smba: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salim Kinje, Ramadhan Chombo/Jonas Mkude, Christopher Edward/Daniel Akuffo, Felix Sunzu na mrisho Ngassa.
    Prisons: 18.David Abdallah, 03.Aziz Sibo, 05.Laurian Mpalile, 16.Lugano Mwangama (Nahodha), 15.David Mwantika, 13.Khalid Fupi, 07.Misango Magai, 12.Fred Chudu/22.Julius Kwaga, 14.Elias Maguri, 17.Peter Michael/Sino Augustino na 19.John Matei/11.Hamisi Ally.

    Nyosso akikabiliana na Peter Michael

    Simba wakishangilia bao la kusawazisha

    Maftah akimdhibiti Maguri

    Hatari langoni mwa Simbam, lakini salaam

    Maguri akitafuta mbinu za kumtoka Shomary Kapombe

    Maftah akiokoa

    Maftah anaokoa

    Maftah anaokoa mbele ya Maguri

    Hatari langoni mwa Simba

    Kaseja anaokota mpira nyavuni, bao la Maguri

    Juma Nyosso anapambana na Maguri

    11 wa Simba leo

    Nyosso na Peter Michael

    11 wa Prisons walioanza leo

    Nyosso na Peter Michael

    DUWA LA KUKU; Prisons wakisali kabla ya mechi

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WATUMA SALAMU YANGA, WAWAPIGA MAAFANDE WA PRISONS TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top