• HABARI MPYA

    Sunday, September 30, 2012

    HATIMAYE BOBAN ATIA TIMU ZENJI

    Boban

    Na Mahmoud Zubeiry
    HATIMAYE kiungo tegemeo wa Simba SC, Haruna Moshi Shaaban, ameungana na wenzake jioni hii kambini visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yangas SC, Jumatano.
    Boban hakucheza mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Prisons kwa sababu alikuwa anasumbuliwa na homa ya matumbo na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa alikuwa anajisikilizia afya yake.
    Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
    Morali ya kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3, kuanzia sa 1:00 usiku.
    Simba inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2:00 leo kumenyana na All Stars ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na mpambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga..
    Simba imerejea leo Zanzibar, baada ya jana kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa, nne.
    Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zikwishafungana bao 1-1, Prisons wakitangulia kupata bao dakika ya sita baada ya Maguri kuwatoka mabeki wa Simba kupiga shuti lililomgonga Shomary Kapombe na mpira kupoteza mwelekeo na kumchanganya kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja na kutinga nyavuni.
    Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Prisons waliendelea kuwa wagumu, hadi walipojisahau kidogo sekunde za mwishoni za kipindi cha kwanza na Felix Sunzu akatumia pasi ya Amiri Maftah kusawazisha dakika ya 45.
    Kipindi cha pili, Simba walirudi na moto na kuanza moja kwa moja kulishambulia mfululizo lango la Prisons na dakika ya 55 Ngassa akafunga kwa shuti dhaifu, ambalo kipa wa Prisons, David Abdallah alidaka lakini mpira ukamtoka na kuingia nyavuni.
    Mechi hiyo ilichezeshwa na refa, Paul Soleji kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo, mshika kibendera namba moja, Mwarabu Mumba mshika kibendera namba mbili, wote kutoka Morogoro, wakati refa wa Akiba alikuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam. 
    Dakika ya 87 Amir Maftah alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Khalid Fupi wa Prisons, hivyo ataukosa mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumatano na hiyo ni nafasi kwa chipukizi Paul Ngalema.
    Hiyo inakuwa kadi ya pili nyekundu kwa Simba ndani ya mechi nne, awali katika mechi ya pili dhidi ya JKT Ruvu, Emmanuel Okwi alilimwa kadi ya aina hiyo kwa kumpiga kiwiko Kessy Mapande na akafungiwa mechi tatu.
    Kikosi cha Simba jana kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salim Kinje, Ramadhan Chombo/Jonas Mkude, Christopher Edward/Daniel Akuffo, Felix Sunzu na mrisho Ngassa.
    Prisons: 18.David Abdallah, 03.Aziz Sibo, 05.Laurian Mpalile, 16.Lugano Mwangama (Nahodha), 15.David Mwantika, 13.Khalid Fupi, 07.Misango Magai, 12.Fred Chudu/22.Julius Kwaga, 14.Elias Maguri, 17.Peter Michael/Sino Augustino na 19.John Matei/11.Hamisi Ally.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMAYE BOBAN ATIA TIMU ZENJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top