• HABARI MPYA

  Saturday, March 02, 2019

  TAMBWE ATOKEA BENCHI KUIPA USHINDI YANGA SC, YAICHAPA ALLIANCE FC 1-0

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Yanga SC imeendelea kuwapa raha mashabiki wake baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 64 baada ya kucheza mechi 26, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC wanaofuatia kwenye nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi SImba SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 48 za mechi 19.
  Haukuwa ushindi mwepesi, kwani pamoja na kucheza vizuri wakimiliki zaidi mpira, lakini Yanga SC walilazimika kusubiri hadi dakika ya 74 kupata bao leo pekee la ushindi,
  Bao hilo limefungwa mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Joselyn Tambwe dakika 10 na ushei baada ya kuingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya kiungo mkongwe wa kimataifa wa Tanzania, Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’.


  Tambwe alifunga bao hilio kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Heritier Ebenezer Makambo ambaye naye alipokea pasi nzuri ya mchezaji mwenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kiungo Papy Kabamba Tshishimbi aliyekutana na mpira uliorudi kufuatia majaro iliyoingizwa na beki Kelvin Yondan kutoka upande wa kulia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomari Lawi kutoka Kigoma, mapema dakika ya sita Makambo alikosa penalti baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa John Mwanda kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa na Siraj Juma.
  Refa Lawi akakataa bao la Alliance FC lililofungwa na Bigirimana Blaise dakika ya 63 kwa sababu aliyetengeneza nafasi hiyo, Sameer Vincent alikuwa ameotea.
  Wachezaji wa Alliance walimlalamikia refa huyo chipukizi mara mbili kwa kuwanyima penalti baada ya wachezaji wa Yanga kunawa mpira kwenye boksi na baada ya mchezo walimfuata kumzonga wakimlalamikia zaidi kwa uchezeshaji wake uliowasaidia zaidi wapinzani wao jioni ya leo. 
  Kikosi cha Alliance FC kilikuwa; John Mwanda, Israel Patrick, Siraj Juma, Wema Sadoki, Geofrey Luseke, Juma Nyagi, Sameer Vincent/Richard John dk80, Balama Mapinduzi, Bigirimana Blaise, Hussein Javu/Michael Chinedu dk58 na Dickson Ambundo.
  Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa ‘Banka’ dk61, Haruna Moshi ‘Boban’/Amissi Tambwe dk61, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Deus Kaseke/makapu dk81.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Ruvu Shooting imeichapa mabao 6-2 Mwadui FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Mshambuliaji Fully Zulu Maganga amefunga mabao matatu dakika za 12, 28 na 69 huku mabao mengine ya Ruvu yakifungwa na Emmanuel Martin dakika ya 13, Tumba Lui Swedi dakika ya 20 na Mussa Said dakika ya 22, wakati ya Mwadui FC yamefungwa na Salim Aiyee dakika ya tatu na Wallace Kiango dakika ya 60.
  Uwanja wa Meja Isamuhyo, bao pekee la Ally Ahmed ‘Shiboli’ dakika ya sita likaipa ushindi wa 1-0 JKT Tanzania dhidi ya Coastal Union ya Tanga, wakati KMC leo imelazimishwa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMBWE ATOKEA BENCHI KUIPA USHINDI YANGA SC, YAICHAPA ALLIANCE FC 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top