• HABARI MPYA

    Monday, March 11, 2019

    MBWANA SAMATTA ASAINI MKATABA MPYA KRC GENK HADI MWAKA 2021

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji hadi Juni mwaka 2021.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Ubelgiji, Samatta amesema kwamba alisaini mkataba huo Januari mwaka huu.
    “Ndiyo, nimesaini mkataba mpya wa mwaka zaidi kuendelea kuichezea KRC Genk na sasa nitakuwa mchezaji wa klabu hiyo kwa miaka mitatu zaidi hadi mwaka 2021 mwezi Juni, amesema Nahodha huyo wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

    Mbwana Samatta amesaini mkataba mpya KRC Genk hadi Juni mwaka 2021

    Samatta mwenye umri wa miaka 26, alijiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuisaidia kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    Hadi sasa, Samatta amekwishaichezea Genk jumla ya mechi 144 za mashindano yote na kufunga mabao 59, kati ya hizo 24 za Europa League ambako amefunga mabao 14, 111 za Ligi ya Ubelgiji na kufunga mabao 44 na kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili.
    Kwa sasa Samatta anaongoza kwa mabao katika Ligi ya Ubelgiji msimu huu, akiwa amefunga mabao 20, moja tu kwa penalti akifuatiwa kwa mbali na mkongwe wa Tunisia, Hamdi Harbaoui wa Zulte-Waregem mwenye umri wa miaka 34 aliyefunga mabao 16.

    Mbwana Samatta kwa sasa anaongoza kwa mabao kwenye Ligi ya Ubelgiji

    Anashika nafasi ya tatu kwa wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye Ligi za Ulaya, nyuma ya Muargentina Lionel Messi wa Barcelona aliyefunga mabao 26, manne kwa penalty kwenye La Liga na Mfaransa Kyllian Mbappe wa PSG aliyefunga mabao 24, moja kwa penalty kwenye Ligue 1.
    Samatta analingana na Mtaliano Fabio Quagliarella wa Sampdoria aliyefunga mabao 20 pia, lakini sita kwa penalty kwenye Serie A, akifuatiwa na Cristiano Ronaldo wa Juventus aliyefunga mabao 19, matano kwa penalti.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBWANA SAMATTA ASAINI MKATABA MPYA KRC GENK HADI MWAKA 2021 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top