• HABARI MPYA

  Tuesday, March 05, 2019

  MAREFA WA DRC NDIYO KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA SC NA JS SAOURA JUMAMOSI ALGERIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na wenyeji, JS Saoura Jumamosi Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar utachezeshwa na marefa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Hao ni Jean-Jacques Ndala Ngambo atakayepuliza kipyenga na mshika kibendera namba moja Olivier Safari Kabene, wakati mshika kibendera wa pili Soulaimane Amaldine anatokea Comoro.
  Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka leo jioni mjini Dar es Salaam kwenda Algeria kupitia Dubai kwa ajili ya mchezo huo wa mchezo wa marudiano, baada ya Januari 12 Simba SC kushinda 3-0 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

  Simba SC itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na AS Vita ya DRC Machi 16 Dar es Salaam kujaribu kulipa kisasi cha kufungwa 5-0 Kinshasa Januari 19.
  Kwa sasa, Al Ahly ambayo wikiendi itakuwa mgeni wa AS Vita mjini Kinshasa ndiyo inaongoza Kundi D kwa pointi zake saba, moja zaidi ya Simba SC baada ya timu zote kucheza mechi nne.
  JS Saoura yenye mshambuliaji Mtanzania, Thomas Ulimwengu inashika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi moja na Simba SC na yenyewe ikiizidi pointi moja AS Vita inayoshika mkia.
  Mechi za wikiendi hii Bechar na Kinshasa zinatarajia kutoa taswira ya timu zitakazofuzu kwenda Robo Fainali kutoka kundi hilo, ingawa picha halisi inaweza kupatikana baada ya mechi za mwisho kabisa Machi 16.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAREFA WA DRC NDIYO KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA SC NA JS SAOURA JUMAMOSI ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top