• HABARI MPYA

  Friday, March 01, 2019

  AZAM FC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI CHINI YA CHECHE, YAICHAPA AFRICAN LYON 3-1

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 53 katika mechi ya 26, ikiendelea kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Yanga SC yenye pointi 61 za mechi 25 na mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 48 za mechi 19.
  Hali ni mbaya kwa African Lyon iliyo katika msimu wake wa kwanza tu tangu irejee tena Ligi Kuu, ikibaki na pointi zake 21 baada ya kucheza mechi 28, hivyo kuendelea kushika mkia kwenye ligi ya timu 20.

  Wachezaji wa Azam FC wakipongezana kwa ushindi wao dhidi ya African Lyon 

  Mabao ya Azam FC leo yamefungwa na Obrey Chirwa dakika ya saba, Mudathir Yahya dakika ya 65 na Rolland Msonjo aliyejifunga dakika ya 90, wakati bao pekee la African Lyon limefungwa na Baraka Jaffar dakika ya 15.
  Huo ni mchezo wa pili Azam FC inacheza na kushinda chini ya kocha wa muda, Iddi Nassro Cheche baada ya kufukuzwa kwa Mholanzi, Hans van der Pluijm na Msaidizi wake, mzawa Juma Mwambusi.
  Mchezo wa kwanza ulikuwa ni wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Jumatatu wiki hii ambao walishinda 3-0 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora.  
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nne; Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Alliance FC watawakaribisha Yanga SC, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting watawakaribisha Mwadui FC, Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni, JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Coastal Union na Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, KMC watawakaribisha Biashara United.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI CHINI YA CHECHE, YAICHAPA AFRICAN LYON 3-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top