• HABARI MPYA

  Wednesday, August 15, 2018

  YANGA SC YAENDELEA KUTOA ADHABU MORO…LEO WAMEIPIGA 1-0 MKAMBA RANGERS KILOSA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeendelea kufanya vyema katika mechi zake za kujipima nguvu kwenye kambi yake ya Morogoro baada ya leo pia kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mkamba Rangers wilayani Kilosa.
  Pongezi kwa kiungo mtaalamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),  Papy Kabamba Tshishimbi aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 83 katika mchezo ambao wenyeji waliwabana mno vigogo wa nchi.
  Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera aliwaanzisha Beno Kakolanya, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Papy Kabamba Tshishimbi, Eritier Makambo, Raphael Daudi na Deus Kaseke.

  Kipindi cha pili akawainua beki Pato Ngonyani, Said Juma ‘Makapu’, Yussuf Mhilu, Pius Buswita na Juma Mahadhi na ndipo bao lilipopatikana.
  Huo ulikuwa mchezo wa tatu mfululizo Yanga inashinda 1-0 mkoani Morogoro, kwanza ikiichapa Mawenzi Market kwa bao la Makambo na juzi ikiibwaga Kombaini ya Kilosa kwa bao pekee la Simon Gustavo aliyepandishwa kutoka timu ya vijana.
  Yanga imerejea Morogoro mjini baada ya mchezo huo, kuendelea na kambi yake ya kujiandaa na mchezo wa Jumapili wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria. 
  Wakati huo huo: Zoezi la kutoa fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi Yanga SC limeanza rasmi leo makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam.
  Hiyo ni baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti, Yussuf Manji Mei mwaka jana, Makamu wake, Clement Sanga mwezi uliopita na Wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji kwa vipindi tofauti.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEA KUTOA ADHABU MORO…LEO WAMEIPIGA 1-0 MKAMBA RANGERS KILOSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top