• HABARI MPYA

    Friday, August 31, 2018

    UCHAGUZI MKUU WA TASWA KUFANYIKA NOVEMBA 25

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Utendaji ya Chama Cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), iliyokutana Dar es Salaam jana Agosti 30 imepanga Uchaguzi Mkuu wa chama hicho ufanyike Novemba 25 mwaka huu.
    Kikao kimekubaliana sekreterieti iwasiliane na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwajulisha uamuzi huo na kuomba chama kiruhusiwe kifanye uchaguzi kwa kutumia katiba ya zamani, hivyo suala la marekebisho ya Katiba ambalo BMT iliagiza lifanyike litafanywa na uongozi utakaoingia madarakani.
    Kutokana na hali hiyo watakaoshiriki uchaguzi huo ni wanachama wote wa TASWA waliopo katika leja kuanzia Juni mwaka 2004 hadi Juni mwaka 2017, wakiwemo walioingia uanachama wakati wa semina ya waandishi chipukizi iliyofanyika Dar es Salaam Oktoba mwaka 2014 na sharti ni kila mwanachama kulipia ada ya mwaka mmoja.

    Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto (kushoto) akiwa na Katibu wake Mkuu, Amir Mhando (kulia)

    Pia kikao kimekubaliana kupokea wanachama wapya, ambao ni waandishi wa habari za michezo na wanakidhi vigezo vya kuwa wanachama kwa mujibu wa Katiba ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya mwaka mmoja, nao wataruhusiwa kushiriki mkutano wa uchaguzi na kupiga kura.
    Kwa mazingira hayo Kamati ya Utendaji imemteua Gift Macha kuratibu suala la waandishi wa habari za michezo wanaotaka uanachama na itampa maelekezo ya utaratibu unaotakiwa, wakati wanachama wa zamani watapaswa kulipia ada zao kwa Mhazini Msaidizi, Zena Chande kuanzia Jumatatu Septemba 3 na mwisho wa kulipia ada kwa wanachama wapya na wale wa zamani itakuwa Oktoba 5, mwaka huu.
    "Tunawaomba wote wenye nia njema ya kuijenga TASWA yetu wahamasishane kuwa wanachama kwa kulipia ada, ili wapate nguvu ya kushiriki katika vikao vya uamuzi," amesema Katibu wa TASWA, Amir Mhando katika taarifa yake.
    Uongozi wa sasa wa TASWA uliingia madarakani mwaka 2014, ambapo Juma Pinto alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Egbert Mkoko (Makamu Mwenyekiti), Amir Mhando (Katibu Mkuu), Grace Hoka (Katibu Mkuu Msaidizi), Shija Richard (Mhazini) na Zena Chande (Mhazini Msaidizi).
    Wajumbe ni Rehure Nyaulawa, Chacha Maginga, Mussa Juma, Mwani Nyangassa, Mroki Mroki, Ibrahim Bakari na Majuto Omary anayeingia kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa TASWA FC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UCHAGUZI MKUU WA TASWA KUFANYIKA NOVEMBA 25 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top