• HABARI MPYA

    Tuesday, August 28, 2018

    FIFA YAIRUHUSU SIMBA KUMTUMIA CHAMA, WAZAMBIA WAAMBIWA WAFUNGUE KESI...DIDA NAYE SAFI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limeipa Simba SC kibali cha muda cha kumtumia kiungo Mzambia, Cletus Chama kufuatia klabu yake, Dynamos ya Lusaka kugoma kufanya hivyo.
    Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba SC zimesema kwamba FIFA imewaandikia TFF, Shirikisho la Soka Tanzania wairuhusu klabu hiyo kumtumia Chama hadi hapo hapo suala lake litakapopatiwa suluhu na  kupatiwa Hati rasmi ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
    Pamoja na kukamilisha taratibu zote za usajili wake Simba SC, akisaini mkataba wa miaka miwili, lakini Dynamos imegoma kumpa Chama ITC ikidai inamdai fedha kulingana na makubaliano yao nje ya mkataba.

    FIFA imeipa Simba SC kibali cha muda cha kumtumia kiungo Mzambia, Cletus Chama (kushoto)

    Na baada ya FIFA kupelekewa kesi hiyo, imeiagiza TFF imruhusu Chama kuendelea kucheza Simba SC kulinda kipaji chake, huku ikiitaka Dynamos kuwasilisha kesi juu ya malalamiko.
    Katika hatua nyingine, Simba SC imefanikiwa kupata ITC ya kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyekuwa anachezea timu ya Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.
    Na baada ya kufanikiwa kutatua matatizo ya kiusajili ya wachezaji wake hao wawili, Simba SC imeiandikia barua TFF na Bodi ya Ligi ikiomba iruhusiwe kucheza mechi yake ya Septemba 1, mwaka huu dhidi ya Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Hiyo ni baada ya Bodi kuahirisha mechi tatu, nyingine zikiwa ni kati ya Azam FC na Ruvu Shooting ya Pwani Septemba 1, Uwanja wa Azam Complex na Septemba 2 kati ya Mwadui FC na Yanga SC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Mechi hizo zimeahirishwa kwa sababu ya wachezaji wengi wa Azam, Simba na Yanga kuchaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania na Uganda ‘The Cranes’ mjini Kampala Septemba 8, mwaka huu.
    Simba SC inaamini kwa kikosi chake kipana haitaathirika kucheza bila kipa wake namba moja, Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya na Hassan Dilunga na mshambuliaji na Nahodha, John Bocco.
    Wachezaji wa Yanga SC waliopo kwenye kikosi cha kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike ni Benno Kakolanya, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum wakati wa Azam FC ni beki ni Aggrey Morris na mshambuliaji Yahya Zayed.
    Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YAIRUHUSU SIMBA KUMTUMIA CHAMA, WAZAMBIA WAAMBIWA WAFUNGUE KESI...DIDA NAYE SAFI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top