• HABARI MPYA

    Saturday, August 25, 2018

    PLUIJM AELEKEZA NGUVU ZAKE KWA NDANDA BAADA YA KUWAPIGA MBEYA CITY MECHI YA KWANZA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Mholanzi Hans van der Pluijm amefurahishwa na ushindi dhidi ya Mbeya City usiku wa juzi na sasa anaelekeza nguvu zake kwenye mchezo ujao dhidi ya Ndanda FC Jumatatu usiku pia
    Azam FC ilianza vema mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuifunga Mbeya City, 2-0 mabao ya kiungo Joseph Mahundi na mshambuliaji Danny Lyanga, ushindi uliowawezesha kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi tatu na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.
    “Nashukuru kila mchezaji ameonyesha hiko kitu nimeshawaambia nina wachezaji 25 kikosini na wakati huu wachezaji wawili hawapo ambao ni majeruhi katika upande mwingine wote wanaweza kucheza na hakuna anayefikiria kama yupo chini au hana kiwango kila mmoja anaweza kucheza na hiko ndicho wameonyesha.

    Mholanzi Hans van der Pluijm akiwa na wasaidizi wake, Juma Mwambusi (katikati) na Iddi Abubakar (kulia)

    “Nina furaha sana kuna ari ya kujitoa kwenye timu na uwajibikaji mzuri kati ya vijana,” alisema kocha huyo aliyeinoa Singida United msimu uliopita, huku akionyesha sura yenye furaha.
    Kuelekea mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumatatu ijayo saa 2.00 usiku, Pluijm alisema kuwa wanatakiwa kujiandaa vema kutokana na mchezo huo kuwa mgumu.
    “Tutapumzika siku moja kesho (leo), tutakayotumia kwa ajili ya kuwarejesha vema wachezaji (recovery), Jumamosi jioni tutafanya mazoezi, Jumapili jioni tutafanya mazoezi na Jumatatu tunatakiwa kuwa tayari kwa mpambano mwingine.
    “Angalia ukisema itakuwa mechi rahisi, mimi nitakuwa nimedanganya kwa sababu mechi zote zinatarajia kuwa ngumu nilieleza mwanzoni kwenye mahojiano haya, kila mmoja anataka kuonyesha kitu dhidi ya Azam, Simba na Yanga,” alisema.
    Mholanzi huyo aliongeza kuwa: “Nafikiri kuna wachezaji wengi wanataka kucheza hapa haitakuwa uwezo wa kuonyesha wa mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima kama unavyoona walivyopambana (Mbeya City) hadi dakika ya mwisho.”   
    Wachezaji wa Azam FC waliokuwa majeruhi hadi sasa ni beki Yakubu Mohammed na mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye anamalizia programu ya mwisho ya kujiweka fiti baada ya kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu. Beki Daniel Amoah, naye anaendelea vema kuuguza majeraha yake ya goti yatakayomuweka nje ya dimba hadi Februari mwakani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM AELEKEZA NGUVU ZAKE KWA NDANDA BAADA YA KUWAPIGA MBEYA CITY MECHI YA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top