• HABARI MPYA

    Wednesday, August 22, 2018

    AZAM FC WATARAJIA KUANZA LIGI KUU NA REKODI NZURI...WANAMENYANA NA MBEYA CITY KESHO CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itaanza kampeni ya kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kwa kuvaana na Mbeya City kesho ikiwa na bonge la rekodi la kujivunia.
    Azam FC itamenyana na wabishi hao wa jiji la Mbeya, katika mchezo wake wa kwanza wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
    Matajiri hao wa viunga vya Azam Complex, wataingia dimbani wakiwa wanashikilia rekodi ya kuwa timu pekee inayoanza kampeni ya kuwania taji la ligi msimu huu ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika mechi saba za mwisho za ligi hiyo ilizocheza nyumbani msimu uliopita.
    Katika mechi hizo saba za mwisho za nyumbani, Azam FC imeshinda mara sita ikizichapa Ndanda (3-1), Singida United, Mwadui (zote 1-0), Mbao (2-1), Majimaji (2-0), Tanzania Prisons (4-1) na kutoa sare mmoja dhidi ya Njombe Mji (0-0).
    Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mchezo wa nyumbani kwenye ligi, ilikuwa ni miezi saba iliyopita ilipofungwa na Yanga mabao 2-1 (Januari 27, 2018), bao la Azam FC likifungwa na Shaaban Idd, aliyehamia Club Deportivo Tenerife ya Hispania.
    Kwa mujibu wa takwimu, rekodi hiyo inaonyesha kuwa Azam FC ni timu ngumu hasa inapotumia uwanja wake wa nyumbani kwani katika mechi 15 za ligi ilizocheza Azam Complex msimu uliopita, imeshinda mechi 11, ikipata sare tatu na kufungwa mmoja.
    Hivyo rekodi hiyo inaibeba Azam FC dhidi ya Mbeya City, licha ya mechi nyingi za timu hiyo kuwa na ushindani hasa wanapocheza ndani ya dimba hilo linalomilikiwa na matajiri hao, ambao wametoka kutwaa taji la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) kwa mara ya pili mfululizo ikiifunga Simba mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali.
    Kihistoria timu hizo zimekutana mara 10 kwenye ligi, tokea timu hiyo ya jijini Mbeya ilivyopanda daraja mwaka 2013, Azam FC ikiwa imeshinda asilimia 95 ya mechi zote ikiibuka kidedea mara tano, sare nne na kupoteza mara moja.
    Mchezo ilioupoteza ilitokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka pointi tatu Azam FC baada ya kushinda mabao 3-0 jijini Mbeya, ikidai ilimchezesha beki Erasto Nyoni kimakosa kutokana na mchezaji huyo kukusanya kadi tatu za njano.
    Katika mechi tano kati ya hizo zilizopigwa Azam Complex, Azam FC imeshinda mara mbili huku mechi tatu zikienda nguvu sawa, ambapo sare inayokumbukwa a wengi ilikuwa ni ile ya mabao 3-3 msimu wa 2013/2014, Azam FC ikifanikiwa kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza.
    Mbali na kufanya usajili mzuri katika dirisha hili, ikiwanasa mabeki Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, ikimrejesha kiungo wake Mudathir Yahya, na kuongeza silaha nyingine kama washambuliaji Tafadzwa Kutinyu, Danny Lyanga, Ditram Nchimbi na Donald Ngoma, Azam FC imeimarisha benchi lake la ufundi ikiwachukua makocha wazoefu na ligi, Mholanzi Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WATARAJIA KUANZA LIGI KUU NA REKODI NZURI...WANAMENYANA NA MBEYA CITY KESHO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top