• HABARI MPYA

    Friday, August 31, 2018

    AMUNIKE AWASAMEHE WACHEZAJI SIMBA SC LAKINI AKATAA KUWAREJESHA KAMBINI MECHI NA UGANDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike amekataa kuwarejesha kambini wachezaji sita wa Simba SC waliokaidi kuripoti kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8 mjini Kampala.
    Pamoja na hayo, Amunike amesema kwamba amewasamehe wachezaji hao baada ya kikao cha pamoja kati ya klabu yao, Simba SC na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juzi jioni. 
    Mnigeria huyo amesema milango iko wazi kwa Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na John Bocco kwenye mchezo mwingine wa Taifa Stars iwapo wataendelea kufanya vizuri katika klabu zao.

    Nyota hao wa klabu bingwa Tanzania, pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum wameenguliwa Taifa Stars kwa utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kuripoti kambini kwa muda uliotakiwa.
    Na baada ya kuwaondoa Kapombe, Nyoni, Mkude, Kichuya, Dilunga, Bocco na Feisal katika kikosi kinachojiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, Amunike  amewachukua mabeki, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar. 
    Taifa Stars iliingia kambini Jumanne wiki hii katika hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam na inafanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani.
    Wachezaji walioripoti kambini hadi sasa pamoja na walioongezwa ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Benno Kakolanya wa Yanga SC na Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC, Aggrey Morris, kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC.
    Nyota wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili kuanzia kesho ambao ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Himid Mao wa Petrojet FC ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa, Shaaba Iddi wa CD Tenerife  ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, Emmanuel Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
    Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema Agosti, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE AWASAMEHE WACHEZAJI SIMBA SC LAKINI AKATAA KUWAREJESHA KAMBINI MECHI NA UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top