• HABARI MPYA

    Sunday, August 26, 2018

    MANJI AMERUDI YANGA NA KLABU BADO INAENDELEA ‘KUTEMBEZA BAKULI’

    KAMPENI za kuhamasisha wapenzi na wanachama kuichangia klabu ya Yanga zinaendelea vizuri nchini zikiongozwa na Televisheni ya Azam TV.
    Hiyo ni kutokana na kile kinachoaminika hali ya kifedha ndani ya klabu ni mbaya, kwa sababu haina mfadhili baada ya kujiuzuli kwa Mwenyekiti, Yussuf Manji.
    Jumapili iliyopita Manji aliibuka hadharani baada ya muda mrefu na kwa ujumla tangu ajiuzulu, akiingia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wakati wa mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.
    Manji alizunguka Uwanja wa Taifa kusalimia mashabiki kabla ya kwenda kwenye vyumbani kuzungumza na wachezaji na baadaye kupanda jukwaani kutazama mechi – Yanga ikashinda 2-1 dhidi ya USM Alger.

    Manji alijiuzulu Mei mwaka jana Yanga, lakini mkutano wa wanachama wa Juni 10, mwaka huu Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam ulikataa ombi lake la kujiuzulu na kusema unaendelea kumtambua kama Mwenyekiti.
    Tangu hapo inafahamika jitihada za kumshawishi akubali kurudi madarakani zimekuwa zikiendelea, lakini Manji hajawahi kutoa tamko, au taarifa kama ilivyo kawaida yake japo akiahidi siku moja atarejea madarakani, au atarejesha msaada wa kifedha.
    Na Jumapili Manji hakuna sehemu alisema amerudi Yanga, zaidi tu ya kuonekana alikuja kujumuika na wana Yanga wenzake kutazama mechi.
    Hayo yakiendelea, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema wachezaji wapo katika mwezi wa nne wa kufanya kazi bila kupata mishahara. Wachezaji wengi wamesajiliwa kwa mali kauli. Klabu ina madeni mengi. Na harambee za michango zimeshika kasi.
    Tayari wana Yanga wengi wamekwishaamini kwamba kuonekana kwa Manji Uwanja wa Taifa Jumapili iliyopita ni mwisho wa matatizo. Magazeti yetu nayo yanavyopamba, basi ni kama tayari mambo safi tena Yanga.
    Na matokeo ya ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya USM Alger na Mtibwa Sugar 2-1 pia mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu, nayo yanaongeza imani kwamba mambo safi tena Yanga.
    Kweli mambo safi Yanga? Kweli Manji amerejea Yanga katika hadhi nafasi aliyokuwa nayo wakati anajiuzulu, au alijitokeza kutoa hamasa japo mashabiki waanze kwenda utena wanjani baada ya kuombwa sana?
    Haijulikani. Hakuna  anayeweza kuujua ukweli kwa sababu Manji hajatoa tamko kuhusu mustakabali wake Yanga, jambo ambalo linazidi kuwaweka watu wengi njia panda.
    Kama Manji amerudi inakuwaje bado klabu inatembeza bakuli kuomba misaada ya fedha? Hilo ndilo swali la kujiuliza kwa sababu ilipofikia Yanga watu wanahitaji kujua mustakabali wa klabu yao.
    Watu wanataka sana Manji arudi kama Mwenyekiti na mfadhili pia, lakini je yeye mwenyewe yupo tayari? Na kama yupo tayari kuna tatizo gani kuutangazia umma wa wana Yanga kama amerudi kuliko kuendelea kuaminishwa vitu ambavyo havieleweki?
    Ni aibu kwa klabu kubwa kama Yanga kutegemea kuchangiwa fedha ili kujiendesha, maana yake viongozi wameshindwa kuisaidia klabu na zinahitajika jitihada za haraka kuinusuru katika hali hiyo.  
    Yanga SC inahitaji uongozi kwanza, bada ya aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga tangu Mei mwaka jana alipojiuzulu Manji naye kujiuzulu mwezi uliopita.
    Hiyo ni baada ya Sanga na Manji kuingia madarakani Yanga katika uchaguzi uliofanyika Julai 15, mwaka 2012 na matokeo kutangazwa Alfajiri ya siku iliyofuata ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga mjini Dar es Salaam.
    Sanga aliyepigiwa debe na Manji, alipata kura 1948 dhidi ya 475 za Yono Kevela na 288 za Ayoub Nyenzi katika uchaguzi amabo Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na Geroge Manyama walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Nao hao waliingia madarakani kupitia uchaguzi mdogo, ulioitishwa baada ya viongozi wote wa juu, Mwenyekiti Lloyd Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha kujiuzulu pia.
    Baada ya safu hiyo kumaliza muda wake, Juni 12, mwaka 2016 ukafanyika uchaguzi mwingine na wote wawili wakatetea nafasi zao, Manji ambaye hakuwa na mpinzani alipata kura 1,468 kati ya 1,470 na Sanga alipata 1,428 kati ya 1,508 akimshinda Tito Osoro aliyepata kura 80.
    Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji, idadi ya kura zikiwa kwenye mabano ni Siza Augustino Lymo (1027), Omary Said Amir (1069), Tobias Lingalangala (889), Salum Mkemi (894), Ayoub Nyenzi (889), Samuel Lukumay (818), Hashim Abdallah (727) na Hussein Nyika (770).
    Hao waliwashinda David Luhago (582), Godfrey Mheluka (430), Ramadhani Kampira (182), Edgar Chibura (72), Mchafu Chakoma (69), George Manyama (249), Bakari Malima 'Jembe Ulaya' (577), Lameck Nyambaya (655), Beda Tindwa (452), Athumani Kihamia (558), Pascal Lizer (178) na Silvester Haule (197).  
    Lakini katika awamu zote mbili, Sanga alionekana kuwa na kazi nyepesi kutokana na nguvu ya Mwenyekiti wake, Manji kiuchumi, utendaji na ushawishi – mambo yalianza kuwa magumu Yanga na kwa Sanga baada ya Manji kujiuzulu Mei mwaka jana baada ya miaka 11 akianza kama mfadhili mwaka 2006.
    Limekuwa pigo kubwa kuondoka kwa Manji Yanga, ambaye alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Kamati ya Utendaji kutoka uongozi uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua mno baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti mwenyewe, Yussuf Manji na Wajumbe wa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika na bado haijafahamika mustakabali wa klabu ni upi, zaidi harambee za kuichangia timu zimeshika kasi wakati tayari watu wamekwishaaminishwa Manji amerudi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI AMERUDI YANGA NA KLABU BADO INAENDELEA ‘KUTEMBEZA BAKULI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top