• HABARI MPYA

    Thursday, August 23, 2018

    MAKAMBO AENDELEA KUFANYA MAMBO YANGA SC IKIIADHIBU MTIBWA SUGAR 2-1 TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeanza vyema Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo wa pili mfululizo baada ya Jumapili kuichapa USM Alger 2-1 pia katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika unamaanisha Yanga si timu ya kubeza katika msimu mpya.
    Mabao ya Yanga SC leo yalipatikana kipindi cha kwanza yote, yakifungwa na mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eritier Makambo na Nahodha Kelvin Yondan kwa penalti, wakati la Mtibwa lilifungwa na Haroun Chanongo.
    Mtibwa Sugar waliuanza mchezo vizuri na kuutawala kwa takriban robo saa, kabla ya Yanga SC kuzinduka na kuanza kucheza vyema.
    Wachezaji wa Yanga wakifurahia bao lao la pili, lililofungwa na Nahodha Kelvin Yondan. Kulia ni mfungaji wa bao la kwanza, Eritier Makambo 
    Eritier Makambo akifunga bao lililokataliwa ambalo lingekuwa la kwanza 
    Deus Kaseke (kulia) akijaribu kumpita Cassian Ponera wa Mtibwa Sugar
    Mrisho Ngassa wa Yanga (kulia) akipiga hesabu za kumpita Cassian Ponera wa Mtibwa Sugar

    Makambo alifunga bao zuri dakika ya 23 kwa kichwa, lakini refa Meshack Suda wa Singida, aliyekuwa anasaidiwa na Sylvester Mwanga wa Kigoma na Geoffrey Msakila wa Geita akakataa bao hilo.
    Wana Jangwani hao hawakukata tamaa na juhudi zao zikawalipa dakika ya 32, Makambo tena akifunga kwa kichwa tena akimalizia krosi ya beki wa kushoto Gardiel Michael.
    Beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ akamuangusha mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa kwenye boksi na Yondan akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 40.
    Kipindi cha pili Yanga SC walikianza vizuri tena na Makambo akapoteza nafasi mbili nzuri za kufunga akiwa amebaki na kipa Benedictor Tinocco, mara zote akikosa hesabu nzuri za kumchenga mlinda mlango huyo.
    Na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Chanongo akauwahi mpira uliopanguliwa na kipa Benno Kakolanya kuifungia bao pekee Mtibwa Sugar leo.
    Bao hilo likawazindua Yanga na kuanza tena kupeleka mashambulizi langoni mwa Mtibwa Sugar, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi. 
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Stand United imeichapa 1-0 African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati, KMV imelazimisha sare ya 0-0 na JKT Tanzania Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mchezo kati ya Azam FC na Mbeya City unaendelea Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kukamilisha mechi za ufunguzi za Ligi Kuu zilizoanza jana. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Benno Kakolanya, Juma Abdul/Said Juma ‘Makapu’ dk89, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Deus Kaseke, Feisal Salum, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Mrisho Ngassa/Raphael Daudi dk65.
    Mtibwa Sugar; Beneditor Tinoco, Ally Shomari, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Cassian Ponera, Hassan Isihaka, Shaaban Nditi, Ismail Aidan, Henry Joseph/Riffat Khamisi dk53, Kelvin Sabato, Awadh Juma na Salum Kihimbwi/Haroun Chanongo dk67. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAKAMBO AENDELEA KUFANYA MAMBO YANGA SC IKIIADHIBU MTIBWA SUGAR 2-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top