• HABARI MPYA

  Sunday, August 19, 2018

  YANGA SC YACHEZA VYEMA NA KUICHAPA USM ALGER 2-1 MBELE YA MANJI…MAKAMBO MTU KWELI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuilaza mabao 2-1 USM Alger ya Algeria usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inapanda nafasi ya tatu katika Kundi D ikifikisha pointi nne baada ya kufungwa mechi tatu awali na kutoa sare moja – kuelekea mchezo wa mwisho wa ugenini dhidi ya Rayon Sport nchini Rwanda wiki ijayo.
  Katika mchezo wa leo, Yanga SC ilionyesha mabadiliko makubwa ya kichezaji baada ya muda mrefu wa kucheza ovyo na kuwaudhi mno mashabiki wake.
  Ikiongozwa kwa mara ya kwanza na kocha wake mpya, Mkongo Mwinyi Zahera, Yanga SC ilipata bao lake la kwanza dakika ya 43 kupitia kwa kiungo Deus Kaseke aliyetumia makosa ya mabeki wa USM Alger na kumchambua kipa Mohammed Lamine.
  Wafungaji wa mabao ya Yanga SC leo, Eritier Makambo (kulia) na Deus Kaseke (kushoto)
  Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Deus Kaseke akimtoka mchezaji wa USM Alger 
  Mfungaji wa bao la pili la Yanga, Eritier Makambo akimtoka beki wa USM Alger  
  Kiungo wa Yanga, Raphael Daudi akiuwahi mpira dhidi ya mchezaji wa USM Alger  

  Hiyo ilifuatia USM Alger kutawala mchezo kwa takriban dakika zote 30 za mwanzo na kulitia kwenye misukosuko lango la Yanga iliyoongozwa na Nahodha wake mpya, Kelvin Yondan katika safu ya ulinzi.
  Kipindi cha pili Yanga SC walirudi vizuri na kufanikiwa kupata bao la pili mapema tu, mfungaji mshambuliaji wake mpya, Mkongo Heritier Makambo dakika ya 47 aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa baada ya shuti lake mwenyewe la kwanza kufuatia pasi ya Juma Mahadhi. 
  Bao hilo likawapa Yanga SC hamu ya kusaka mabao zadi na hiyo ikawagharimu kuwaruhusu wageni kupata bao lao pekee lililofungwa na Abderrahmane Meziane dakika ya 53.
  Yanga SC wakarekebisha makosa yao na kuendelea kutawala tena mchezo wakilishambulia mfululizo lango USM Alger, lakini umaliziaji mbaya ukawanyima walichokuwa wakikitafuta.
  Mapema kabla ya mchezo huo kuanza, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji aliingia uwanjani na kuzunguka majukwaa akisalimia mashabiki kabla ya kwenda kuzungumza na wachezaji vyumbani kisha kupanda jukwaani kutazama mchezo.
  Manji alijiuzulu Mei mwaka jana na kuacha hali ngumu katika klabu, kwani pamoja na kuwa Mwenyekiti, pia alikuwa ndiye mfadhili mkuu wa Yanga.
  Bado hajatoa tamko rasmi kama amerejea au la, kufuatia mkutano wa wanachama wa Juni 10 mwaka huu kukataa ombi lake la kujiuzulu. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Benno Kakolanya, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Deus Kaseke, Papy Kabamba Tshishimbi, Eritier Makambo, Pius Buswita/Juma Mahadhi dk46/Ibrahim Ajib na Raphael Daudi/Thaban Kamusoko dk84.
  USM Alger: Mohammed Lamine, Doris Mixes/Aymen Mahious dk51, Farouk Chafai, Faouzi Yaya, Abderrahmane Meziane/Amir Sayoud dk67, Prince Vinny Ibara, Abderrahim Hamra, Mohammed Maftah/Mehdi Benchikhoune dk38, Hemza Koudri, Mokhtar Benmoussa na Abderaouf Benguit.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YACHEZA VYEMA NA KUICHAPA USM ALGER 2-1 MBELE YA MANJI…MAKAMBO MTU KWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top