• HABARI MPYA

    Wednesday, August 15, 2018

    REFA BORA LIGI KUU KUCHEZESHA MECHI YA NGAO YA JAMII JUMAPILI MWANZA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa Ngao ya Jamii kati ya Simba SC na Mtibwa Sugar ya Morogoro Jumapili Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza utachezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Elly Sasii wa Dar es Salaam.
    Msemaji wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amesema kwamba Sasii atasaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Hellen Mduma wa Dar es Salaam, wakati refa wa akiba atakuwa Jeonesya Rukyaa wa Kagera.   
    Ndimbo amesema kwamba Mtathmini wa waamuzi katika mchezo huo atakuwa refa mstaafu wa kimataifa, Alfred Lwiza wa Mwanza, wakati Kamisaa ni Said Soud wa Tanga.
    Elly Sasii ndiye atachezesha mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba SC na Mtibwa Sugar Jumapili Uwanja wa Jamhuri mjini Mwanza 

    Simba SC, mabingwa wa Ligi Kuu watakuwa wanacheza mechi ya kuwania Ngao kwa mara ya sita kihistoria, wakati kwa Mtibwa, washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC) watakuwa wanafanya hivyo kwa mara ya pili tu tangu kuanzishwa kwa mchuano huo mwaka 2001.
    Simba SC waliandika historia nyingine katika soka ya Tanzania, baada ya kuwa moja ya timu mbili za kwanza kucheza mechi ya kwanza Ngao mwaka 2001 walipofungwa 2-1 ma mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
    Mchuano huo ukasimama kwa kukosekana mdhamini hadi uliporejea mwaka 2009 na Mtibwa Sugar wakawa mabingwa wa pili baada ya kuwachapa Yanga SC 1-0 Uwanja wa Uhuru.
    Simba SC wakashindwa kutwaa tena Ngao mwaka 2010 baada ya kufungwa kwa penalti 3-1 na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufuatia sare ya 0-0 Uwanja mpya wa Taifa.
    Michuano ya nne ya Ngao ya Jamii mwaka 2011 ndiyo iliipa Simba SC ushindi wa kwanza wa taji hilo, baada ya kuilaza Yanga SC 2-0 Uwanja wa Taifa kabla ya Wekundu hao wa Msimbazi kubeba tena ‘Ubao’ mwaka uliofuata, 2012 baada ya kuifunga Azam FC 3-2.
    Yanga SC wakabeba Ngao ya Jamii mara tatu mfululizo mara zote wakiifunga Azam FC, mwaka 2013 bao 1-0, mwaka 2014 mabao 3-0 na mwaka 2015 kwa penalti 8-7 kufuatia sarte ya 0-0.
    Azam FC wakatwaa Ngao yao pekee ya Jamii mwaka 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 na mwaka jana, Simba SC wakawapiga mahasimu wao wa jadi kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
    Kwa mara ya kwanza kihistoria, Jumamosi wiki hii mechi ya Ngao ya Jamii itafanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam na Mwanza imekuwa na bahati hiyo wakizipokea Simba SC na Mtibwa Sugar kupenua pazia la Ligi Kuu msimu wa 2018-2019. Nani ataibuka mshindi? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REFA BORA LIGI KUU KUCHEZESHA MECHI YA NGAO YA JAMII JUMAPILI MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top