• HABARI MPYA

  Sunday, August 19, 2018

  NGAO YA JAMII ILIKUWA HALALI YAO SIMBA SC, LAKINI…

  MABINGWA wa Tanzania, Simba SC jana wamefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Hiyo inakuwa mara ya nne kwa Simba SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya mwaka 2011 wakiifunga Yanga 2-0, mwaka 2012 wakiifunga Azam FC 3-2 na mwaka jana wakiwafunga tena mahasimu wao wa jadi, kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
  Katika mchezo wa jana uliochezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Elly Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma wote wa Dar es Salaam, na Ferdinand Chacha wa Mwanza, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
  Mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere alianza kuifungia Simba SC dakika ya 29 kwa shuti kali kutokea pembezoni mwa Uwanja kushoto, baada ya kuwatoka mabeki wa Mtibwa Sugar na kipa wao, Benedictor Tinocco kufuatia kazi nzuri ya Hassan Dilunga.
  Kelvin Sabato Kongwe au Kiduku akaisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 33 baada kupokea pasi nzuri ya Saleh Hamisi na kufumua shuti zuri akiwa anatazamwa na mabeki wa Simba SC.
  Wakati refa Sasii anajiandaa kupuliza filimbi ya kukamilisha kipindi cha kwanza, Hassan Dilunga akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya dakika 45 stahili za mchezo.
  Dilunga aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar mwezi uliopita tu baada ya awali kuchezea Ruvu Shooting, Yanga SC na JKT Ruvu, alifunga bao hilo kwa shuti lililowababatiza wachezaji wengine kufuatia pasi ya Mganda, Emmanuel Okwi.
  Kipindi cha pili mchezo uliendelea kupendeza, Simba SC wakisaka mabao zaidi na Mtibwa Sugar wakitafuta bao la kusawazisha lakini hakuna timu iliyofanikiwa kutikisa nyavu. 
  Ulikuwa mchezo mzuri na baada ya kambi ya wiki mbili Uturuki, maandalizi mazuri ya kumalizia kabla ua kuingia kwenye msimu mpya ikiwemo mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana, Namungo za Arusha United za hapa – Simba SC walistahili ushindi.
  Walistahili ushindi kwa sababu waliwekeza katika maandalizi, kuanzia kambi ya Uturuki na hata timu iliporejea ikapitia mechi tatu za kukipima kikosi, wakitoa sare mbili, 1-1 na Kotoko Uwanja wa Taifa, 0-0 na Namungo Uwanja wa Majaliwa na kushinda 2-1 dhidi ya AU.
  Kama Simba SC ingepoteza mechi ya jana ingewavuruga mno kuanzia mfadhili wao, Mohammed Dewji, viongozi na benchi la Ufundi – kwa sababu wasingeiona thamani ya maandalizi yao yaliyowafikisha hadi Ulaya.
  Simba SC imesajili vizuri, karibu kila nafasi ina wastani wa wachezaji wawili na wote wazuri – zaidi kikosi kina uwiano mzuri wa wachezaji wakongwe, vijana na kuna chipukizi pia.
  Ukiwatazama wachezaji kama Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Haruna Niyonzima na John Bocco ukasema  ‘wazee’, lakini kuna vijana wadogo wengi akina Abdul Salim, Yussuf Mlipili, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mohammed Rashid, Adam Salamba na Rashid Juma.
  Lakini sehemu kubwa ya wachezaji wa Simba ni wa umri wa wastani wa ukomavu wa kucheza soka na kuhimili mikikimikiki hapo unawazungumzia akina Aishi Manula, Nicolas Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga, Muzamil Yassin, Shomari Kapombe, Said Ndemla, Shiza Kichuya na Cletus Chama.
  Wakiwa mabingwa wa Tanzania, Simba SC watashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani na bila shaka watapenda kufanya vizuri kuendeleza rekodi ya tangu miaka ya 1970.
  Na kuelekea msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa, maandalizi yameanza vizuri kwa usajili wa kikosi chenye mseto mzuri wa wachezaji kwa umri, lakini pia ni wengi ni wachezaji kweli. Pongezi kwa Simba SC, ushindi wa Ngao ya Jamii ni halali yao, lakini tu wasibweteke msimu ndiyo kwanza unaanza – kuna Ligi Kuu ya timu 20.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGAO YA JAMII ILIKUWA HALALI YAO SIMBA SC, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top