• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2018

    AMUNIKE BILA MAANDALIZI NA WACHEZAJI WALIO TAYARI NI KAZI BURE

    KATIKA wiki ambayo nyota wawili wa zamani wa La Liga, kiungo mshambulijai Clarence Clyde Seedorf na mshambuliaji Patrick Stephan Kluivert, wote Waholanzi walikuwa wanatambulishwa kuwa makocha wa timu ya taifa ya Cameroon, nchini Tanzania nako kulikuwa kuna tukio kama hilo.
    Nyota mwingine wa zamani wa La Liga, winga Emmanuel Amunike aliyecheza Barcelona kati ya mwaka 1996 hadi 2000, alikuwa anatambulishwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hii, Taifa Stars.
    Cameroon imemchukua Seedorf aliyecheza Real Madrid kati ya 1996 na 2000 kama kocha Mkuu na Kluivert ambaye alicheza Barcelona kuanzia 1998 hadi 2004 kama Msaidizi wake, wakati Tanzania Amunike aliyesaini mkataba wa miaka miwili atakuwa kocha Mkuu wa timu zote za taifa akisaidiwa na wazawa. 

    Na siku mbili baada ya utambulisho wake, nilikutana naye kwa mahojiano ambayo yalichapishwa katika tovuti hii wiki hii.
    Katika mahojiano hayo, Amunike alisema kwamba hakuja Tanzania kufanya miujiza, bali anachowahakikishia wapenzi wa soka wa nchi hii ni kwamba atajaribu na kujituma, kwa sababu anfahamu kujituma kutawafikisha sehemu, kwani huo ndio ufunguo wa mafanikio.
    Lakini kwa ujumla anaonekana ni mtu aliye tayari kwa kazi na ana nia ya kuitumia fursa hii ya kufundisha timu ya kwanza ya wakubwa ya taifa kwa kupata mafanikio ili aingie katika orodha ya makocha bora wa kimataifa. 
    Amunike mwenye umri wa miaka 47, aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    Mayanga aliiongoza Taifa Stars kwa mara ya mwisho Machi 27, mwaka huu ikishinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Siku hiyo, mabao ya Tanzania yalifungwa na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
    Taifa Stars inakuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
    Japokuwa Taifa Stars ndiyo timu yake ya kwanza ya taifa ya wakubwa, lakini Amunike mwenye umri wa miaka 47 amefundisha klabu za Al Hazm kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 aliporejea nyumbani kufunisha Ocean Boys.
    Alipoachana na U17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.  
    Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
    Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini kabla ya mwaka 2003 kwenda kumalizia soka yake Busan I'Cons alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan.
    Kwa uzoefu wa kuanzia kuwa mchezaji mkubwa wa kimataifa wa Nigeria aliyecheza klabu kubwa za Ulaya na baadaye kuwa kocha wa timu za vijana za kwao na klabu mbalimbali barani, Amunike ni mwalimu sahihi kabisa kwa Taifa Stars.
    TFF imepatia kwa Amunike – lakini kuleta kocha ni jambo moja, bado yanahitajika maandalizi kwa ajili ya timu, kuhakikisha kocha anatekelezewa programu zake na wachezaji wanafurahia maisha yao ya kambini kwenye timu za taifa, ikiwa ni pamoja na kupewa posho zao kwa wakati.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE BILA MAANDALIZI NA WACHEZAJI WALIO TAYARI NI KAZI BURE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top