• HABARI MPYA

    Sunday, October 22, 2017

    YANGA WAANZA KUTETEA UBINGWA, WAITANDIKA STAND UNITED 4-0 SHINYANGA, HAJIB AFUNGA MAWILI

    Na Salma Suleiman, SHINYANGA
    YANGA SC wameonyesha wapo tayari kutetea ubingwa, baada ya leo kuwafumua mabao 4-0 wenyeji Stand United kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Shujaa wa Yanga leo amekuwa mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga mabao mawili na kuseti moja, lililofunga na Obrey Chirwa wakati bao lingine la wana Jangwani hao limefungwa na kiungo Pius Buswita.
    Kwa matokeo hayo, Yanga inafikisha pointi 15 baada ya kucheza mechi saba na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakizidiwa kwa wastani wa mabao tu ya kufunga na kufungwa na Simba SC wenye pointi 15 pia sawa na Mtibwa Sugar walio nafasi ya tatu. 
    Ibrahim Hajib amefunga mabao mawili na kuseti moja Yanga ikishinda 4-0 leo


    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka kutoka Arusha aliyesaidiwa na Omary Juma na Vincent Mlabu, Stand United walikaribia kupata bao dakika ya kwanza tu baada ya shuti la mpira wa adhabu la Hamad Kibopile kumchomoka mikononi kipa Mcameroon wa Yanga, Youthe Rostand ambaye hata hivyo aligeuka haraka na kuukamata kabla haujavuka mstari.
    Yanga wakafunguka na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Stand United na haikuwa ajabu walipomaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ibrahim Hajib Migomba.
    Hajib alifunga bao la kwanza kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 24 kutoka upande wa kushoto akipiga kwa mguu wake wa kulia na kipa Frank Muwonge akaupangulia juu mpira ukagonga mwamba wa juu na kudondokea chini nyavu ndogo kulia.
    Bao la pili lilitokana na kazi nzuri ya mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa ambaye aliwachukua na kuwapiga chenga ya pamoja mabeki wawili wa Stand United upande wa kulia ndani kidogo jirani na boksi kabla ya kutia krosi kwa mguu wa kulia ambayo ilimkuta Hajib akiwa amedhibitiwa na walinzi wawili, lakini akatuliza mpira na kufumua shuti kufunga dakika ya 30.
    Kipindi cha pili Yanga walirudi na kiu yao ya mabao na kufanikiwa kufunga mara mbili tena, Buswita akianza dakika ya 53 kufunga kwa kichwa baada ya kona ya winga Geoffrey Mwashiuya akitumia mwanya wa kuachwa peke yake na mabeki wa Stand waliokuwa wamemdhibiti Hajib wakati huo.
    Chirwa akafuatia dakika ya 69 akitumia makosa ya kipa Frank Muwonge kutoka bila mahesabu langoni mwake na kuuruhusu mpira uliopigwa na Hajib udunde, Mzambia wa Yanga akaupitia na kupiga shuti haraka kuelekeza nyavuni mwa Stand United kuipatia timu yake bao la nne.
    Ushindi huu mnono wa kwanza kwa Yanga msimu huu pamoja na kiwango kizuri cha uchezaji unakuja wiki moja kabla ya mchezo dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba Oktoba 28 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga inatarajiwa kwenda kisiwani Pemba kesho kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wao ujao dhiid ya Simba.
    Kikosi cha Stand United leo kilikuwa; Frank Muwonge/Mohammed Makaka dk73, Aaron Lulambo, Hamad Kibopile, Erick Mulilo, Ally Ally, Rajab Rashid, Ambros James/Morris Mahela dk67, John Mwitiko, Adam Salamba, Wisdom Mutasa na Emmanuel Kitoba/Bakari Mohammed dk42.
    Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Pato Ngonyani, Pius Buswita, Papy Tshishimbi, Obrey Chirwa/Yussuf Mhilu dk77, Ibrahim Hajib/Mussa Said dk71 na Geoffrey Mwashiuya/Emmanuel Martin dk82.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAANZA KUTETEA UBINGWA, WAITANDIKA STAND UNITED 4-0 SHINYANGA, HAJIB AFUNGA MAWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top