• HABARI MPYA

    Tuesday, October 10, 2017

    MLANGO WA UANI WAIPONZA SIMBA, YATOZWA FAINI NUSU MILIONI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeitoza faini ya Sh 500,000 klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
    Taarifa ya Kamati kwa Bin Zubeiry Sports – Online imesema kwamba kitendo hicho cha Simba ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia Kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba.
    Nayo klabu ya Singida United imepigwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
    Adhabu dhidi ya Singida United imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu, wakati kitendo cha mashabiki wao ni kosa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu.
    Nayo Stand United imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba, zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Katika mechi namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu, mashabiki hao waliwafanyia vurugu wachezaji wa Mbeya City wakati wakielekea vyumbani baada ya mchezo kumalizika, kabla ya Polisi kuingilia kati na kuwatawanua.
    Adhabu hiyo ambayo ni sh. 500,000 (laki tano) kwa kila mechi imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Kamati imeionya klabu ya Stand United endapo vitendo hivyo vitatokea tena haitasita kuichukulia hatua kali zaidi za kikanuni.
    Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na wachezaji wake kuvaa jezi zenye namba tofauti na zile zilizosajiliwa. Wachezaji hao walivaa namba tofauti kwenye mechi namba 40 dhidi ya Simba iliyofanyika Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Stand United ilikiuka Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu inayelekeza kuwa kila mchezaji atatumia namba ya kudumu ya jezi iliyosajiliwa na klabu yake wakati wa maombi ya usajili. Adhabu dhidi ya Stand United ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.
    Kamati pia imemuondoa Mwamuzi Msaidizi Grace Wamara kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa kukosa umakini na kutomsaidia Mwamuzi, hivyo kusababisha akubali bao lenye utata la Stand United dhidi ya Mbeya City.
    Wamara alikuwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili kwenye mechi hiyo namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na wenyeji Stand United kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
    Uamuzi wa kumuondoa Wamara ambaye amerejeshwa katika Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya hatua nyingine umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MLANGO WA UANI WAIPONZA SIMBA, YATOZWA FAINI NUSU MILIONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top