• HABARI MPYA

    Sunday, May 07, 2017

    SIMBA YAREJEA ANGA ZA UBINGWA…YAILAMBA LYON 2-1

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu y Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo uliotokana na mabao ya Ibrahim Hajib na beki wa Lyon, Hamad waziri aliyejifunga, unawafanya Wekundu wa Msimbazi wafikishe pointi 62 baada ya kucheza mechi 28 wakiwarudisha nafasi ya pili, mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 59 za mechi 26.  
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Ludovic Charles wa Tabora aliyesaidiwa na Robert Luhemeja wa Mwanza na Vincent Mlabu wa Morogoro, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
    Wachezaji wa Simba wakimpongeza Ibrahim Hajib baada ya kufunga bao la kwanza leo


    Ibrahim Hajib akimtoka beki wa African Lyon leo
    Beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa African Lyon, Rehani Kibingu
    Kiungo wa Simba, Mghana James Kotei akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Lyon, Rehani Kibingu
    Winga wa Simba, Shizza Kichuya akifumua shuti mbele ya wachezaji wa Lyon

    Mshambuliaji Ibrahim Hajib alitangulia kuifungia Simba kwa shuti la mbali lililombabatiza beki wa Lyon, Hassan Isihaka na kutinga nyavuni dakika ya 37 baada ya kupokea pasi ya kiungo Muzamil Yassin. 
    Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika nane tu, kabla ya kiungo wa Lyon, Omar Abdallah kuisawazishia timu yake kwa shuti la mbali pia lililowapita mabeki wa SImba na kipa wao, Mghana, Daniel Agyei.
    Kipindi cha pili Simba wakakianza vizuri tena na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 54  kufuatia bekki wake, Hamad Waziri kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kichwa wa mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo. 
    Baada ya bao hilo, Simba walianza kucheza kwa kujihami zaidi kuulinda ushindi wao, huku Lyon wakipambana kutafuta bao la kusawazisha bila mafanikio.   
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Mwinyi Kazimoto dk62, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Frederick Blagnon dk86 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Juma Luizio dk65.
    African Lyon; Youth Rostand, Miraj Adam, Omar Salum, Hamadi Waziri, Hassan Isihaka, Baraka Jaffar, Rehani Kibingu/Abdallah Mguhi dk63, Peter Mwalyanzi, Thomas Maurice, Venence Ludovic/Awadh Juma dk75 na Omar Abdallah.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAREJEA ANGA ZA UBINGWA…YAILAMBA LYON 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top