• HABARI MPYA

  Sunday, May 07, 2017

  MALINZI AWAFARIJI WAFIWA VIFO VYA WANAFUNZI, WALIMU ARUSHA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa rambirambi ya Sh 500,000 kwa walengwa walipoteza watoto katika ajali ya gari iliyoua zaidi ya watu 36, wakiwamo wanafunzi 33.
  Wanafunzi hao 33 wa darasa la saba, walimu wawili na pamoja na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vicent ya Arusha, walifariki dunia jana Mei 6, mwaka huu.
  Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi, vifo hivyo vilivyotokea saa 3 asubuhi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa rambirambi msiba wa wanafunzi na walimu wao Arusha

  Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema ambako kabla ya kufika basi walilopanda liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo hivyo na majeruhi watatu.
  Rambirambi hiyo ya TFF inakwenda sambamba na salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyeungana na viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuomboleza msiba huo.
  Katika salamu zake za rambirambi, Rais Malinzi amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo hivyo kwani imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia taifa katika tasnia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu kama wachezaji, makocha, viongozi hapo baadaye.
  “Mtazamo wetu kwa sasa ni kuendeleza soka la vijana, tena hasa wale walioko mashuleni, hivyo vijana wale ni sehemu ya kutimiza ndoto za TFF katika mpira wa miguu hapo baadaye, tunakubali haya yote kwa kuwa ni ya Mwenyezi Mungu ndiye anayejua siri,” amesema Rais Malinzi.
  Salamu za Rais Malinzi zimekwenda kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, akisema: “Huu ni wakati mgumu kwa Wana – Arusha, wazazi na walezi hawana budi kuwa na subira kwa sasa.”
  Amesema kwamba kwa wanafamilia wote wa mpira wa miguu, “Tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema. Pia wale waliopata majeruhi tunaomba wapone haraka katika ajali hiyo mbaya. Ee Mwenyezi Mungu zipumzishe Roho za Marehemu hao, Mahala pema peponi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AWAFARIJI WAFIWA VIFO VYA WANAFUNZI, WALIMU ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top