• HABARI MPYA

    Sunday, May 07, 2017

    SERIKALI YAPASWA KUELEWA ILIPOFIKIA MABADILIKO LAZIMA SIMBA NA YANGA,

    RAIS wa zamani wa Marekani, John Fitzgerald ‘Jack’ Kennedy aliwahi kusema; “Mabadiliko ni sheria ya maisha. Na wale wanaotazama nyuma na pale walipo tu, hawatasonga mbele,”.
    John F. Kennedy aliyasema hayo katika ukumbi wa mikutano wa Paulskirche mjini Frankfurt, Ujerumani June 25, mwaka 1963 katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye moja ya mikutano mikubwa ya kujadili amani duniani. 
    Lakini kila jambo lazima lije kwa sababu na wakati unapofika mabadiliko huwa ni lazima na mfano ni namna ambavyo Tanzania ilivyoingia kwenye siasa za vyama vingi kwa kulazimisha mwaka 1995 licha ya wananchi kukataa katika kura za maoni.
    Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliishauri Serikali chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kukubali kuingia kwenye demokrasia ya vyama vingi, licha ya wananchi wengi kupinga katika kura za maoni.
    Mwalimu Nyerere alijua kwa nini wananchi wengi walikataa siasa za vyama vingi – na ndiyo maana alipoona chama tawala, CCM kinazidi kuchafuka aliibuka tena kabla ya kifo chake na akawapasha viongozi wake.
    Mwalimu Nyerere alisema, Watanzania wanataka mabadiliko na kama hawatayapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM.
    Leo nataka nielezee umuhimu wa mabadiliko wakati unapowadia na mabadiliko yanayozungumziwa siyo ya kwenye siasa pekee, bali hata kwenye michezo.
    Sera za michezo za taifa zimechakaa, zinahitaji kubadilishwa. Katiba zetu nyingi zimejaa kutu, zinahitaji kubadilishwa kwa ujumla tumepoteza dira na ndiyo manaa michezo nchini inazidi kudidimia.  
    Mwishoni mwa mwaka jana, mijadala ya ubinafsishaji wa klabu kongwe za michezo nchini, Simba na Yanga ilitawala baada ya kujitokeza kwa wafanyabiashara wawili wenye asili za Kiasia, Yussuf Manji na Mohammed Dewji kutaka kuwekeza kwenye klabu hizo.
    Lakini baadhi ya wanachama walipinga na baadaye kikatokea kikwazo kikubwa zaidi, ambacho ni Serikali yenyewe ilipoonekana kuwawekea vikwazo Manji na Dewji kuwekeza kwenye timu hizo. 
    Manji aliomba apewe klabu kwa miaka 10 na katika kipindi hicho atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama.
    Na katika kipindi hicho cha miaka 10, timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini yake Manji.
    Hata hivyo, hilo lilishindikana baada ya Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati.
    Ikumbukwe Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mfadhili awali akitumia kampuni ya Loto Kitita kuidhamini klabu hiyo, wakati huo Mwenyekiti wa klabu akiwa Francis Kifukwe.
    Akasaidia kusuluhisha mgogoro uliokuwapo wa Yanga Kampuni na Yanga Asili kwa gharama kubwa na aliyekuwa mpinzani mkubwa wa uongozi, Mzee Yussuf Mzimba (sasa marehemu) akakubali kukaa kando. 
    Yanga SC yenye umoja bila makundi ikaanza maisha mapya na Wakili Imani Mahugila Madega akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa klabu baada ya mwafaka.
    Baada ya kuingia madarakani, Madega hakuelewana na Manji na wawili hao wakawa wanagombana mara kwa mara.
    Haikushangaza Wakili Madega alipomaliza kipindi chake cha kwanza cha uongozi hakutaka kuendelea na katika uchaguzi uliofuata, Wakili menzake, Lloyd Baharagu Nchunga akamshinda Francis Kifukwe.
    Nchunga akavivaa sawia viatu vya Madega na mwisho wa siku naye kwa misimamo yake akageuka adui wa Manji. Na kwa sababu ya kumeguka kwa Kamati yake ya Utendaji, ikiwemo kuondoka kwa aliyekuwa Makamu wake Mwenyekiti, Davis Mosha, Nchunga akashindwa kupambana na Manji, mwishowe akajiuzulu.
    Ukaitishwa uchaguzi mdogo na Manji akagombea mwenyewe Uenyekiti baada ya kushindwa kufanikisha mipango yake chini ya Mawakili wawili, Madega na Nchunga.
    Pamoja na kuwa Mwenyekiti, lakini bado Manji akaona haitoshi kuifanya iwe atakavyo yeye, kama ambavyo akiwa na nguvu kamili za kimamlaka japo kwa muda fulani.
    Ndipo likaibuka wazo la kuikodisha timu, ambalo mwishowe lilipingwa na likashindikana.
    Upande wa pili, Mo Dewji alitaka kununua asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo kwa Sh. Bilioni 20.
    Mo naye alianza kama mfadhili wa Simba mwaka 1998 kupitia kampuni yao ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) hadi mwaka 2005 walipojitoa.
    Na Mo alijitoa baada ya kuona anatoa fedha nyingi kuisaidia timu, lakini mwisho wa siku akawa hana sauti kwa mujibu wa Katiba.
    Akajaribu awali kushawishi mfumo wa kampuni ya hisa, lakini akapingwa naye akaamua kujitoa kabla ya kwenda kuinunua iliyokuwa Mbagala Market na kuigeuza kuwa African Lyon.
    Hata hivyo, pamoja na kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo, Mo Dewji aliamua kuachana nayo, baada ya kugundua mashabiki wa Tanzania wapo kwa ajili ya Simba na Yanga, hivyo Lyon isingemtengezea faida aliyoitaka.
    Ndipo akaachana nayo, kabla ya kuibuka na wazo la kununua hisa Simba. Wakati umefika tukubali tu Mo Dewji na Manji wana uwezo wa kuanzisha timu zao na zikaweza kushiriki Ligi Kuu bila kuyumba.
    Kama Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ anaweza kuendesha timu, kwa nini Manji na Dewji washindwe?
    Lakini kinachoonekana, wawili hao ni wafanyabiashara ambao wameona fursa kupitia Simba na Yanga na wanataka kuitumia kwa kufanikisha mipango yao.
    Nini woga wa wanachama wa Simba na Yanga katika yenye utawala wa kisheria na dola imara kama ya Tanzania? 
    Nini wasiwasi wa Serikali katika hili la Manji na Dewji kutaka kuwekeza Simba na Yanga?
    Nimesikia fununu za ujio wa kampuni ya Sporti Pesa ndani ya Simba na Yanga, lakini bado nauona umuhimu wa mabadiliko ya kiundeshwaji katika klabu hizo.
    Nasema hivyo kwa sababu timu hizo zimekwishakuwa na udhamini  wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa karibu miaka 10, lakini kutokana na mifumo yake mibovu ya uendeshwaji iliyopitwa na wakati hazikunufaika chochote na baadaye zikarudi kuwa omba omba tena.
    Inawezekana wanachama wa Simba na Yanga wakawa hawataki mabadiliko, lakini inawezekana wakawa wanakataa mabadiliko yenye tija kwa klabu zao.
    Naamini wakati umefika kwa Serikali kufikiria kuwapa nafasi wafanyabiashara hao kuwekeza kwenye klabu hizo, kwani kama alivyosema John F. Kennedy; “Mabadiliko ni sheria ya maisha. Na wale wanaotazama nyuma na walipo tu, hawatasonga mbele,” basi nasi tukubali mabadiliko Simba na Yanga zisonge mbele.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAPASWA KUELEWA ILIPOFIKIA MABADILIKO LAZIMA SIMBA NA YANGA, Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top