• HABARI MPYA

  Monday, May 08, 2017

  MAMBO MATANO MAZITO MALINZI AMEIFANYIA SOKA YA TANZANIA

  Na Freddy Mapunda, DAR ES SALAAM
  Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utafanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo vigogo kadhaa wanatarajiwa kujitosa ili kumpa upinzani Rais wa sasa, Jamal Malinzi.
  Uchaguzi huo utahitimisha awamu ya kwanza ya uongozi wa Malinzi ambaye aliingia madarakani mwaka 2013.
  Kutokana na mambo kadhaa ambayo yanaendelea katika soka la Tanzania kumekuwa na mgawanyiko wa maoni ambapo baadhi ya watu wanataka uongozi wa Malinzi ufikie ukomo mwaka huu.
  Pamoja na hisia hizo, uchunguzi wetu umebaini kwamba kuna mambo matano makubwa ambayo yatamrejesha kigogo huyo madarakani tena kwa ushindi mkubwa.

  Soka ya Tanzania imepiga hatua kubwa mbele chini ya Jamal Malinzi

  Soka la vijana
  Mafanikio makubwa zaidi ya Malinzi katika soka la vijana ni kuiwezesha Serengeti Boys kufuzu katika mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.
  Mashindano hayo yanaanza wikiendi hii nchini Gabon ambapo Serengeti imepangwa katika kundi B na timu za Mali, Angola na Niger.
  Safari ya Serengeti Boys kwenda Gabon ilifanyika ndani na nje ya uwanja.
  Ndani ya Uwanja mambo yalikuwa magumu na timu hiyo ilifungwa na Congo Brazzaville, lakini nje ya uwanja ikashinda.
  Malinzi na jopo lake la uongozi hasa chini ya Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine walipeleka malalamiko ya Congo kumtumia mchezaji aliyezidi umri katika mashindano hayo na baadaye Serengeti ikapewa nafasi.
  Mbali na timu hiyo ya miaka 17, Malinzi ameunda timu nyingine ya vijana chini ya miaka 14 ambayo ipo kambini kwenye kituo cha Alliance Mwanza ikijiandaa na fainali za vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika nchini mwaka 2019.
  Wakati huohuo, katika soka la vijana, Malinzi amefanikiwa kuanzisha Ligi ya Vijana ambayo ilifanyika mwaka jana katika vituo vya Bukoba na Dar es Salaam.
  Licha ya ukosoaji mkubwa kwamba ligi hiyo inaendana na ile kombe la Uhai, ni wazi kwamba Malinzi amejitahidi kuona mashindano hayo muhimu yanafanyika licha ya kuwepo kwa mazingira magumu. 
  Mshambuliaji wa Serengeti Boys, Yohana Oscar Nkomola akimpita beki wa Ghana katika mchezo wa kirafiki Dar es Salaam mwezi uliopita

  Udhamini kuongezeka
  Ongezeko la wadhamini katika Ligi Kuu ya Vodacom ni miongoni mwa mambo ambayo yamfanya kigogo huyo atembee kifuambele.
  Tangu mwaka 2013 kumekuwa na ongezeko kubwa la wadhamini kwa TFF pamoja na timu binafsi.
  Tumeshuhudia Azam TV ikiongeza mikataba miwili katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam HD yaani Azam Sports Federation CUP High Definition, Ligi ya Wanawake na Vijana.
  Katika mikataba hiyo miwili Azam ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.3 Mwaka jana Azam ilisaini pia mkataba mpya wa kuendelea kuonyesha Ligi Kuu kwa miaka mitano ambapo mkataba huo mpya una thamani ya Shilingi bilioni 23.
  Malinzi alipata pia udhamini mpya wa Benki ya Diamond Trust kwa timu za Ligi Kuu huku akipata tena udhamini wa NHIF. Mwaka juzi TFF ilipata pia udhamini wa kampuni za StarTimes na Star Tv katika Ligi Daraja la Kwanza, lakini hali ngumu ya kiuchumi ilizifanya kampuni hizo kuondoka mwaka mmoja tu baadaye. 

  Kocha mzalendo wa Taifa Stars, Salum Mayanga akiwa na nahodha wake, Mbwana Samatta (kulia)

  Makocha wazawa
  Ni ukweli ulio wazi kwamba katika kipindi cha Malinzi kumekuwa na ongezeko kubwa la mafunzo kwa makocha wazawa. Kwa sasa idadi ya makocha wazawa imepanda kwa kiasi kikubwa ambapo hadi Waandishi wa Habari wametumia fursa hiyo ya mafunzo.
  Ni wakati huo ambao tumeshuhudia timu ya Taifa ikirejeshwa katika mikono ya makocha wazawa, Charles Boniface Mkwasa na Salum Mayanga.
  Kabla ya Malinzi, timu ya Taifa ilikaa kwa kipindi cha miaka 10 ikiwa chini ya makocha wa kigeni na mafanikio makubwa zaidi yalikuwa kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) mwaka 2009.

  Simba iliitoa Azam FC katika Nusu Fainali ya Kombe la ASFC

  Kombe la ASFC
  Kurejea kwa kombe la FA ambalo lilikoma kwa miaka 13 ni kazi kubwa ya Field Marshal (Jemedari) Malinzi. Kombe hilo la FA lilifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2003 lakini mwaka juzi lilirejea tena na kuongeza msisimko wa soka nchini. Kwa sasa mashindano hayo yanafahamika kama Azam Sports Federation Cup na kwa mwaka huu yameshirikisha timu 86.
  Timu za Mbao FC na Simba zitakutana katika mchezo wa fainali Mei 28, mwaka huu.
  Mwanahamisi Omar 'Gaucho' aliiwezesha Mlandizi Queens kuandika historia ya kubwa bingwa wa kwanza wa Ligi ya Wanawake Tanzania

  Ligi ya Wanawake
  Soka la Wanawake limekuwa likipigiwa upatu duniani kote na mwaka jana Malinzi alifanya sehemu yake baada ya kuwezesha kuanza kufanyika kwa Ligi ya Wanawake.
  Ligi hiyo ilifanyika kwa makundi ambapo timu sita zilizofanya vizuri zilikwenda katika hatua ya mwisho ambapo zilicheza mechi kusaka bingwa.
  Mashindano hayo licha ya kukosa udhamini yalikuwa na msisimko mkubwa miongoni mwa wapenzi wa soka la wanawake nchini.
  Mbali na hilo, wakati wa uongozi wa Malinzi tumeshuhudia timu ya Taifa ya Tanzania Bara ya Wanawake ‘Kilimanjaro Queens’ ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe wa Chalenji kwa wanawake katika mashindano yaliyofanyika nchini Uganda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAMBO MATANO MAZITO MALINZI AMEIFANYIA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top