• HABARI MPYA

  Sunday, April 16, 2017

  YANGA WAACHWA NA NDEGE ALGERIA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI 12 wa Yanga SC pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa wamebaki mjini Algiers baada ya kuachwa na ndege kufuatia kuchelewa kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Algiers unaojulikana pia kama Uwanja wa Ndege wa Houari Boumediene.
  Wachezaji wanaodaiwa kuachwa ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kevin Yondan, viungo Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Emmanuel Martin na mshambuliaji ni Donald Ngoma.  
  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba amepata taarifa hizo, lakini anajaribu kuwasiliana na Katibu, Mkwasa ili wajue cha kufanya.
  “Ndugu yangu mimi nimezisikia hizo taarifa, lakini bado sijazithibitisha. Najaribu kuwasiliana na Katibu Mkuu Mkwasa hapa ili kwanza kuthibitisha na baada ya hapo kama ni kweli tujue cha kufanya,”amesema Mkemi.     
  Yanga jana imetolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mouloudia Club Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers, Algeria katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.  
  Kwa matokeo hayo, Yanga inatolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
  Kundi lingine la wachezaji wa Yanga limeondoka na ndege ya Emirates kurejea Dar es Salaam kupitia Dubai likiwa na wachezaji saba, ambao ni mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe kupitia Dubai.
  Katika kundi hilo kuna benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.   
  Taarifa zinasema sasa kundi hilo litaondoka huko Jumatano kwa ndege nyingine ya Uturuki na maana yake kambi ya Yanga sasa imegawanyika kuelekea mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Prisons Aprili 22. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAACHWA NA NDEGE ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top