• HABARI MPYA

  Sunday, April 02, 2017

  YANGA HAWAJACHELEWA, WAJIPANGE UPYA

  YANGA inakabiliwa na mtikisiko wa kiuchumi kwa sasa, kufuatia Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kuingia matatizoni na Serikali tangu Februari.
  Hakuna anayejua haswa Manji yuko wapi kwa sasa, zaidi ya tetesi tu kwamba yuko Hospitali ya Aga Ghan anaendelea na matibabu ya moyo chini ya usimamizi wa askari kwa madai akipata ahueni anarudishwa rumande.
  Wiki mbili zilizopita ilikuwa apandishwe kizimbani kwa tuhuma za kumiliki pasipoti mbili, lakini ikadaiwa ilishindikana kwa sababu za afya yake.
  Inadaiwa akaunti za Manji zimefungwa na hawezi kutoa fedha tena, maana yake na klabu haipati fedha tena kutoka kwa mfadhili wake huyo. 
  Na huyo ndiye amekuwa tegemeo la Yanga kiuchumi kwa miaka 11 sasa tangu mwaka 2006.
  Manji ameibeba sana Yanga kwa miaka yote 11, lakini kipindi chote hicho hawakupatikana viongozi wa kuweza kutumia fursa hiyo kuijengea klabu misingi imara ya kiuchumi na si ajabu leo inayumba.
  Ipo dhana kwamba viongozi wote walikwamishwa na Manji mwenyewe kwa madai siku moja alitaka kujimilikisha klabu.
  Na baada ya kuibuka kwa mpango wa Manji kutaka kuikodisha timu kupitia kampuni ya Yanga Yetu, dhana hiyo ikachukuliwa kama ni kweli.
  Lakini bado si sababu ya viongozi wote wa kipindi cha ufadhili wa Manji Yanga kushindwa kuijengea misingi imara ya kiuchumi klabu.
  Waje wote leo wawaambie wana Yanga waliweka mkakati gani wa kuijengea misingi ya kiuchumi klabu ikashindikana kwa sababu ya Manji?
  Ukweli ni kwamba viongozi wote waliopita na waliopo walikuwa na wapo pale kwa ajili ya kuhakikisha timu inasajili na kucheza mashindano.
  Na kwa kuwa hayo ndiyo ambayo wamekuwa wakiyasumbukia, hayajawahi kushindikana – Yanga imesajili wachezaji wazuri, imecheza mashindano na kushinda mataji.
  Maana yake, wangeamua kuligeuza jengo la makao makuu ya klabu kuwa la kitegauchumi kwa namna yoyote ingewezekana.
  Wangeamua kuzikomboa mali za klabu ambazo kwa sasa hati za umiliki wake hazijulikani zilipo mfano jengo dogo la Mafia, ingewezekana.
  Wangeamua kurudisha programu ya soka ya vijana iliyowahi kuinufaisha klabu kwa kuzalisha nyota waliogeuka tegemeo la taifa ingewezekana.
  Wangeamua kutafuta makampuni zaidi ya kuidhamini klabu ingewezekana – mambo mengi yangewezekana kama viongozi wa Yanga wangeyashughulikia.
  Lalini walibweteka na kuona Manji anafanya kila kitu. Anasajili timu, analipa mishahara, anagharamia kambi hadi za Ulaya. 
  Lakini hawakuumiza vichwa vyao kidogo kujiuliza bila Manji mambo yatakuwaje. Ndiyo maana leo Manji yupo hai, Yanga inasulubika kiuchumi na haina nyenzo nyingine zaidi ya kuchangishana michango kama ya harusi na kuomba omba misaada.
  Na misaada yenyewe katika kipindi hiki kigumu cha awamu ya tano ya kuisoma namba imekuwa migumu vile vile kupatikana.
  Ni mambo ambayo nimekuwa nikiandika sana kwa muda mrefu na bahati mbaya yakanigeuka ni kunijengea chuki dhidi ya wana Yanga.
  Waliniona naisakama klabu yao kwa kuiandika mara kwa mara, kumbe nilikuwa nawasaidia kuwaonyesha dira.
  Leo Manji anashindwa kuisaidia Yanga si kwa hiari yake, bali matatizo yanayomkabili huku klabu hina hata Uwanja wa mazoezi.
  Simba ambao wamekuwa na maisha magumu kwa kujiendesha bila mfadhili, wanafanikiwa kuingiza nyasi za bandia nchini.
  Simba sasa wanahangaikia fedha za kukomboa nyasi waende wakazibandike kwenye Uwanja wao wa Bunju. Yanga vipi?
  Hawajachelewa Yanga, wajipange upya kuanzia sasa kuhakikisha wanaanza kuhangaikia kuifanya klabu isimame kwa miguu yake.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA HAWAJACHELEWA, WAJIPANGE UPYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top