• HABARI MPYA

    Saturday, April 01, 2017

    AZAM NA YANGA SHUGHULI PEVU TAIFA LEO

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    BAADA ya mapumziko ya takriban wiki mbili kupisha mechi za michuanao ya klabu barani Afrika zilizozihusu klabu za Azam na Yanga na za kirafiki za timu ya taifa, Taifa Stars, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inarejea leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja tofauti nchini.
    Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabingwa watetezi, Yanga watakuwa na shughuli na Azam FC, wakati Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbeya City wataikaribisha, Ruvu Shooting kutoka Mlandizi, mkoani Pwani.
    Kesho; African Lyon wataikaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Prisons wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine Mbeya, Mwadui FC wataikaribisha JKT Ruvu Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Maji Maji FC wataikaribisha Toto African Uwanja wa Maji Maji Songea.
    Mbio za ubingwa zinaongozwa na Wekundu wa Msimbazi, Simba wenye pointi 55, wakifuatiwa na watetezi wa taji, Yanga wenye pointi 53 baada ya timu zote kucheza mechi 24 na wikiendi hii miamba hiyo ya soka nchini itamenyana na timu zinazowafuatia kwa ubora katika Ligi Kuu, Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi zake 44 na Kagera Sugar iliyo nafasi ya nne kwa pointi zake 42, kufuatia kila timu kucheza mechi 24.
    Yanga na Azam leo zinakutana kwa mara ya 19 katika Ligi Kuu tangu Azam ipande mwaka 2008, huku kila timu ikiwa imeshinda mechi tano na kutoa sare nane kati ya 18 za awali.
    George Lwandamina, kocha Mzambia wa Yanga anakumbuka vizuri Januari mwaka huu alipopigwa mabao 4-0 na Azam katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi na bila shaka leo ni siku ya kisasi. 
    Safu za ushambuliaji za timu zote kesho zitawakosa watu muhimu, Yanga itawakosa washambuliaji wake tegemeo, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma ambao ni majeruhi wakati Azam FC, inayofundishwa na kocha Mromania, Aristica Cioaba itamkosa Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ ambaye naye ni majeruhi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM NA YANGA SHUGHULI PEVU TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top