• HABARI MPYA

    Tuesday, April 12, 2016

    KAPOMBE KUREJEA UWANJANI BAADA YA MIEZI MITATU

    Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
    BEKI tegemeo wa Azam FC, Shomari Kapombe (pichani kulia) atakuwa nje kwa miezi mitatu na maana yake hatacheza tena msimu huu. 
    Beki huyo wa zamani wa AS Cannes ya Ufaransa amelazwa hospitali ya Morningside Mediclinic, Johannesburg nchini Afrika Kusini tangu Alhamisi iliyopita akipatiwa matibabu baada ya kugundulika ana ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu).
    Daktari wa timu ya Azam FC, Juma Mwimbe aliyeambtana na mchezaji huyo Afrika Kusini mesema kuwa kwa mujibu wa taarifa alizopata leo kutoka huku ni kuzidi kuimarika kwa afya ya beki huyo.
    “Tunamshukuru Mwenyenzi Mungu anaendelea vizuri sana, nimeongea naye leo asubuhi na ameniambia anajisikia vizuri sana na maumivu kwenye kifua yamepungua na kubakia kwa umbali sana, mpaka sasa hatujajua atarejea lini nchini kwani bado anaendelea na matibabu,” alisema.
    Mwimbe alisema Kapombe anahitaji mapumziko ya miezi miwili hadi mitatu ili kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida, hivyo atazikosa mechi zote zilizobakia za Azam FC msimu huu na huenda akarejea uwanjani kwenye kipindi cha maandalizi ya msimu ujao.
    Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa na kiwango kizuri msimu huu kwani mpaka sasa ameshaifungia Azam FC mabao 11, nane kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mawili Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja amefunga ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) wakati timu hiyo ikiilaza Bidvest Wits mabao 3-0.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAPOMBE KUREJEA UWANJANI BAADA YA MIEZI MITATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top