• HABARI MPYA

  Wednesday, April 13, 2016

  BARCA WATEMESHWA NDOO YA ULAYA, BAYERN MUNICH WAENDA NUSU FAINALI KWA MBINDE

  BARCELONA imevuliwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 2-0 na Atletico Madrid, zote za Hispania usiku huu Uwanja wa Vicente Calderon mjini Madrid.
  Atletico Madrid wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya awali kufungwa 2-1 Uwanja wa Camp Nou, Barcelona.
  Mabao yote ya timu ya Muargentina Diego Simione leo yamefungwa na Antoine Griezmann dakika ya 36 na lingine kwa penalti dakika ya 88.
  Lionel Messi (kushoto) akiwania mpira dhidi ya beki wa Atletico Madrid, Lucas PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Bayern Munich imefakiwa kwa mbinde kwenda Nusu Fainali baada ya kuitoa Benfica kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 2-2 leo Uwanja wa Luz.
  Mabao ya Benfica yamefungwa na Raul Alonso Jimenez Rodriguez dakika ya 27 na Anderson Souza Conceicao dakika ya 76, wakati ya Bayern iliyoshnda 1-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani wiki iliyopita, yamefungwa na Arturo Vidal dakika ya 38 na Thomas Muller dakika ya 52.
  Arturo Vidal (katikati) akipongezwa na wachezaji wenzake wa Bayern Munich baada ya kufunga PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Atletico Madrid na Bayern Munich zinaungana na Real Madrid ya Hispania na Manchester City ya England katika Nusu Fainali, ambayo droo yake itapangwa Ijumaa. 
  Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro aliipeleka Real Madrid Nusu Fainali jana kwa mara ya sita mfululizo baada ya kufunga mabao matatu yake, ikishinda 3-0 Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid dhidi ya Wolfsburg ya Ujerumani.
  Real imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa 2-0 Ujerumani na Ronaldo alifunga mabao yake katika dakika za 15, 17 na 77 na kufikisha mabao 46 msimu huu kwenye mashindano yote.
  Kevin de Bruyne naye alifunga bao pekee dakika ya 14 Uwanja wa Etihad jana na kuipeleka Manchester Nusu Fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya PSG.
  City imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya wiki iliyopita kulazimisha sare ya 2-2 mjini Paris. Sasa, kocha Manuel Pellegrini anaweza kukutana na mrithi wake mwishoni mwa msimu, Pep Guardiola baada ya Bayern Munich pia kuingia Nusu Fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BARCA WATEMESHWA NDOO YA ULAYA, BAYERN MUNICH WAENDA NUSU FAINALI KWA MBINDE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top