• HABARI MPYA

  Monday, April 04, 2016

  AYA 15 ZA SAID MDOE: ULEVI JUKWAANI NI UJANJA AU UPUMBAVU?

  KIASIcha wiki tatu zilizopita pale Vijana Social Hall Kinondoni wakati wadau na wanamuziki wa dansi wanaongea na Mheshimiwa Nape Nnauye, waziri mwenye dhamana na sanaa ikiwemo muziki wa dansi, nilishuhudia kituko kilichonifanya nianze kuamini kuwa kuna wanamuziki wanautukanisha muziki.
  Mwanamuziki mmoja bingwa wa kuzichambua nyuzi za gitaa la solo na gitaa la kati Amos “Roho ya Nabii” akiwa ameutandika vizuri mtungi (pombe) alianza kufanya ghasia za kipumbavu zilizosababisha wanamuziki wenzake Mjusi Shemboza na Totoo ze Bingwa wamtoe kwa nguvu nje ya ukumbi.
  Kwa bahati nzuri sana mwanamuziki huyo aliyepata kuzitumikia Twanga Pepeta na Mashujaa Band alikuwa ameketi nyuma kabisa kwahiyo hadi anaondolewa ukumbini, mheshimiwa Nape hakubahatika kushuhudia upumbavu wa msanii huyo.

  Huyo ni Amos Roho ya Nabii, msanii aliyejipachika jina kubwa lililojaa utukufu lakini matendo yake kwa siku hiyo yalikuwa ni aibu tupu. Tuachane naye huyo, tuje kwa walengwa wakuu wa mada ya leo – wanamuziki wanaopiga mtungi wa kupindukia wakati wanapokuwa kazini.
  Wakati bendi ya Double M Plus inazinduliwa pale Mango Garden Kinondoni, nikayashuhudia matukio mawili ya kilevi yaliyoniacha hoi kama si kuniduwaza.
  Fundi mitambo wa bendi hiyo alikuwa chini ya kiwango, muziki ukatoka mbovu kuliko uliosikika kutoka kwa bendi zilizosindikiza onyesho hilo, Sikinde na G5 Modern Taarab.
  Kwa bahati nzuri siku ile kulikuwa na mafundi mitambo wengi sana ndani ya Mango Garden na kwa nia njema kabisa wakamfuata fundi wa Double M Plus kujaribu kumsaidia au kubadilishana mawazo, lakini fundi huyo akawa mbishi kupindukia hadi baadae sana pale alipokaripiwa na bosi wake Mwinjuma Muumin ndipo akakubali kusaidiwa na muziki ukarudi katika hali yake ya kuridhisha.
  Baada ya kufuatilia kwa makini na kudodosa huku na kule, nikafahamishwa kuwa kisa cha fundi kuharibu kazi sambamba na ubishi wake wa ajabu kwa mafundi wenzake, ni pombe …alikuwa amelewa, alilewa kazini, kalewa ofisini kwake.
  Lakini kulikuwa na kituko kingine kutoka kwa swahiba wangu wa siku nyingi Rashid Sumuni ambaye naye kiwango chake siku hiyo kilinipa mashaka.
  Kwanza wakati anaitwa jukwaani na Mwinjuma Muumin, aliingia huku anayumba kiaina, nikadhani ni mbwembwe za uzinduzi, lakini alipolishika gitaa na kuanza kulicharaza huku akifanya makosa flani flani yaliyomfanya apishane na wenzake, nikapata hamu ya kutafiti nini kimemsibu Sumini, ni woga wa show? Kapania kupita kiasi au kiwango kimeporomoka? Maskini ya Mungu nikapata jibu lile lile lililomsibu fundi mitambo wao – kwamba na yeye alikuwa kapiga mtungi wa haja.
  Lakini hao sio wa kwanza, ulevi jukwaani ni jambo lililokithiri hususan kwa wanamuziki wa dansi, ukienda karibu kila bendi utawakuta wanamuziki wa aina hiyo, si Sikinde, si Msondo, si Twanga Pepeta, si Akudo Impact, ni tatizo sugu.
  Wako wanaoamini kuwa wanaimudu pombe na badala ya kuinywa kwa kujificha basi watataka kupanda jukwaani na chupa zao za pombe, mtu anapiga kinanda au gitaa huku kilevi chake kiko kando.
  Lakini wako pia ambao hawana hata uwezo wa kusubiri wimbo uishe, watashuka jukwaani na kwenda kubugia pombe zao walizoziacha kwenye meza za wateja wao na kisha kurejea jukwaani wakiamini wamejificha lakini utendaji wao unawafichua kuwa wamelewa … ni kero sana yaani kila mwanamuziki mlevi atakuwa na mbinu na hila tofauti kutegemea na miiko ya bendi.
  Maana kuna bendi hazitaki msanii apande na pombe jukwaani lakini hazina kizuizi cha mwanamuziki kupanda jukwaani akiwa amelewa, halafu zipo bendi  zinazohofia wasanii wake watukutu na kuruhusu wapande jukwaani na chupa zao za pombe ingawa ziko chache ambazo hazikubali yote hayo mawili kutokea.
  Muziki ni kazi kama nyingine, kupanda jukwani ukiwa ‘bwii’ ni kosa kubwa katika kazi, kumnunulia msanii pombe anapokuwa kazini ni kosa kubwa, kiongozi au mmiliki wa bendi kuruhusu pombe au ulevi jukwaani ni kosa kubwa …Wakati huu ambao wanamuziki na wadau wa dansi wanapambana kurejesha heshima ya muziki huo, ni vema tukajiuliza: Pombe na ulevi jukwaani ni ujanja au upumbavu? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: ULEVI JUKWAANI NI UJANJA AU UPUMBAVU? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top