• HABARI MPYA

    Thursday, October 01, 2015

    BOSSOU TAABANI, ALAZWA NA KUFUNGWA ‘DRIPU’, WACHEZAJI YANGA WAPEWA LIKIZO

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Yanga SC, Vincent Bossou jana alizidiwa na ugonjwa wa Malaria, kiasi cha kukimbizwa hospitali mjini Morogoro, ambako alitundikiwa dripu.
    Beki huyo wa kimataifa wa Togo, alianza kusumbuliwa na Malaria juzi wakati timu ikiwa mjini Morogoro kwa maandalizi ya mchezo wake jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar kiasi cha kuwahishwa katika hospitali moja binafsi.
    Katika mchezo huo, uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Yanga SC ilishinda 2-0 kwa mabao ya Malimi Busungu na Mzimbabwe, Donald Ngoma.
    Vincent Bossou akiwa amelazwa jana mjini Morogoro baada ya kuzidiwa na Malaria

    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba Bossou, ambaye amecheza mechi tu kwa dakika 45 dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya mchezo wa kirafiki, kwa sasa anaendelea vizuri.
    Hata hivyo, Muro amesema baada ya ushindi wa jana wachezaji wote wamepewa mapumziko hadi Jumatatu kupisha maandalizi ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwa Kanda  ya Afrika.
    “Unajua wachezaji wetu wengi wapo timu za taifa kuanzia hawa wa hapa Tanzania na wa nje pia akina Amissi Tambwe (Burundi), Haruna Niyonzima (Rwanda), Thabani Kamusoko na Donald Ngoma (wote Zimbabwe) kwa hivyo mwalimu (Hans van der Pluijm) ameona tuwape mapumziko mafupi hata wale wachache waliobaki,”amesema Muro.
    Bossou amecheza mechi moja tu kwa dakika 45 ya kirafiki dhidi ya Mbeya City tangu amesajiliwa Yanga SC

    Aidha, Muro amesema kwamba kiungo Haruna Niyonzima ameondoka leo pamoja na kwenda kujiunga na timu ya taifa, lakini pia kushiriki mazishi ya dada yake.
    Mechi za Ligi Kuu za Simba, Yanga na Azam FC wikiendi hii zimeahirishwa kutokana na klabu hizo kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho kimeingia kambini leo kujiandaa na mchezo dhidi ya Malawi Oktoba 7 na 12 nyumbani na ugenini hatua za awali kufuzu Kombe la Dunia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOSSOU TAABANI, ALAZWA NA KUFUNGWA ‘DRIPU’, WACHEZAJI YANGA WAPEWA LIKIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top