• HABARI MPYA

    Sunday, April 07, 2019

    WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA WENYE VIPAJI KUVIENDELEZA ILI VIWANUFAISHE KIMAISHA

    Na Shamimu Nyaki –WHUSM, ARUSHA
    WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka vijana wenye vipaji vya michezo mbalimbali  kuendelea kuviendeleza kwa kuwa michezo katika dunia ya leo ni ajira.
    Waziri Mkuu ameyasema hayo leo mjini Arusha katika Mashindano ya Riadha ya Sokoine Memorial Marathon yaliyolenga kumuenzi Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Moringe Sokoine aliefariki miaka 35 iliyopita ambapo ameeleza kuwa marehemu Sokoine alikua anapenda sana michezo pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
    “Michezo ni muhimu kwakua inaleta umoja,ushirikiano furaha lakini zaidi katika dunia ya leo ni ajira ya kuaminika hivyo ni lazima vijana mkatumia vipaji mlivyonavyo katika michezo mbalimbali ili muweze  kupata ajira na hatimaye mfanikiwe kama wengine waliofanikiwa kupitia sekta hii”.alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.
    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa mashindano ya riadha ya Sokoine Memorial Marathon mjini Arusha leo 
    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi ya Shilingi Milioni 1, mshindi wa mbio za kilometa 21 kwa wanawake, Failuna Mgata  

    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali, Familia ya hayati Edward Sokoine pamoja kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Sokoine Memorial Marathon 

    Aliongeza kuwa Michezo kwa sasa inatangaza Taifa letu ambapo ametolea mfano wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo hivi karibuni imefuzu kushiriki Michuano ya AFCON itakayochezwa baadae mwezi juni huko nchini Misri,Timu ya Vijana chini ya Miaka 17 “Serengeti Boys” itakayoshiriki Mashindano hayo ambayo yatafanyika hapa nchini kuanzia April 14 -28 mwaka huu ambapo timu hiyo inatakiwa kushinda mechi mbili tuu ili iweze kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Brazili.
    Katika hatua nyingine Mhe.Kassim Majaliwa ameeleza kuwa Serikali itaendelea kumuenzi Hayat Edward Moringe Sokoine kutokana na mchango wake wa kuletea Taifa maendeleo kwa kuhimiza wananchi kujituma, kuwa wazalendo pamoja na kudumisha amani ya nchi.
    Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza amesema kuwa mchezo wa riadha umeendelea kufanya vizuri kimataifa kwakua nchi imepata wawakilishi watakaoshiriki mashindano ya Olimpiki yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2020 huko Tokyo Japan,mashindano ya riadha ya Dunia pamoja na Jumuiya ya Madola.
    Mhe.Shonza ameongeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Chama cha Riadha nchini inaendelea na maandalizi ya mashindano ya riadha ya kimataifa ya All Africa Games,World Championship na African Cross Country Championship ambayo Tanzania ndio itakuwa Mwenyeji.
    “Mchezo huu wa riadha umeitangaza vyema nchi yetu kupitia wanariadha mbalimbali waliofanya vizuri kimataifa ambapo timu yetu ya Taifa ya mbio za nyika ilishiriki mashindano nchini Dernmark na kumaliza katika nafasi ya 8,10 na 11 kupitia wanariadha Failuna Matanga,Emmanuel Ginik,Gabriel Geay na Aliphonce Simbu”.alisema Mhe.Shonza.
    Hata hivyo  Rais wa Chama cha Riadha nchini Mhe.Antony Mtaka amewataka waandaaji wa mbio mbalimbali nchini kuzingatia Sheria na taratibu hususan usajili  wa mbio hizo katika  Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kabla ya kuzitangaza ama kuhamasisha wadau na wananchi kushiriki.
    Naye mshindi wa mbio za Kilometa 21 kwa wanawake Bibi Failuna Matanga amesema kuwa mafaniko anayopata kupitia riadha ni kutokana na kujituma kufanya mazoezi pamoja na nidhamu katika mchezo huo.
    Mbio hizo za Soikone Memorial Marathon zilishirikisha mbio za Kilometa 2 na nusu,Kilometa 05  na kilometa 21 ambapo Watoto,wasichana na wavulana walishiriki na washindi kupewa zawadi ikwemo pesa pamoja na medali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA WENYE VIPAJI KUVIENDELEZA ILI VIWANUFAISHE KIMAISHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top