• HABARI MPYA

    Tuesday, April 23, 2019

    YANGA SC YATOZWA FAINI SH. MILIONI 3.5, YONDAN AFUNGIWA NA FAINI 500,000

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh. Milioni 3 kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC Aprili 4, mwaka huu Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
    Taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imesema kwamba hilo ni kosa la nne kwa Yanga SC msimu huu kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14 (49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Aidha, Yanga pia imetozwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani baada ya mechi hiyo kumalizika.
    Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Naye beki wake, Kelvin Yondani amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 
    Taarifa ya Kamati ya Saa 72 imesema kwamba adhabu hiyo ni imezingatia Kanuni ya 38 (9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Naye beki Aggrey Morris wa Azam FC amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Mbao FC katika mechi hiyo ya Aprili 7 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Mchezaji mwingine wa Azam, Paul Peter amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Mbeya City FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 14 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Nayo Ndanda FC imetozwa faini ya Sh. 1,500,000 kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi kwa sababu hilo ni kosa la kwanza kwao msimu huu. 
    Adhabu dhidi ya Ndanda pia ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Nayo Namungo FC imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Friends Rangers FC kugomea mchezo huo uliofanyika Aprili 13 kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani Lindi. 
    Hadi mchezo huo unavunjwa na Mwamuzi kutokana na timu ya Friends Rangers kutoka uwanjani, Namungo FC ilikuwa ikiongoza mabao 2-0.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YATOZWA FAINI SH. MILIONI 3.5, YONDAN AFUNGIWA NA FAINI 500,000 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top