• HABARI MPYA

    Friday, April 26, 2019

    WACHEZAJI YANGA SC WAKUBALI KUANZA MAZOEZI KESHO BAADA YA MAZUNGUMZO NA UONGOZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa Yanga SC wamemaliza mgomo wao baada ya mazungumzo na Kamati ya Usimamizi wa timu chini ya Mwenyekiti, Lucas Mashauri asubuhi ya leo Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam.
    Kikao baina ya wachezaji na viongozi kilifanyika wakati Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwafanyisha mazoezi wachezaji wa timu ya vijana, maarufu kama Yanga B.
    Viongozi wamewaahidi wachezaji kuwapa posho za mechi tatu zilizopita (100,000 kila mechi) kesho watakapoingia kambini na kwamba suala la mishahara na fedha zao za usajili waendelee kufanya subira, kwa sababu kwa sasa klabu haina fedha.

    Na kuhusu ombi kwamba walipwe kutokana na fedha za michango inayoendelea hivi sasa, viongozi wamesema fedha hizo haziwezi kuguswa hadi utakapopatikana uongozi mpya baada ya uchaguzi wa mei 5 mwaka huu.
    Lakini wakawaahidi kabla ya safari ya Iringa kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) watapewa posho za mechi nyingine mbili zilizopita.   
    Hivyo kesho kikosi cha kwanza cha Yanga kitarejea mazoezini Uwanja wa Polisi, Kurasini kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu.
    Mgomo wa wachezaji Yanga ulianza jana wakati walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi, lakini wakawaagiza Manahodha wao, Ibrahim Ajibu na Juma Abdul waende kumuambia kocha Zahera kwamba hawatafanya mazoezi kwa sababu viongozi wamewapuuza.
    Na hiyo ni baada ya juzi wachezaji hao kumuomba Zahera ambaye pia ni kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC awaite viongozi kwenye mazoezi ya leo asubuhi ili wajadiliane juu ya stahiki zao.
    Lakini kitendo cha kutotokea kwa kiongozi hata mmoja mazoezini jana kiliwaudhi wachezaji na kukubaliana kuondoka bila kufanya mazoezi.
    Na Kocha Zahera alionyesha msimamo wa kutotaka kujadiliana chochote na wachezaji zaidi ya kuwaamrisha waingie uwanjani kufanya mazoezi. Mwishowe, wachezaji wakaondoka na kocha naye na Maafisa wake wa benchi la Ufundi wakaondoka kinyonge.
    Baadaye kocha Zahera alimuagiza Mratibu wa timu, Hafidh Saleh awatumie ujumbe wachezaji wote kuwaambia wasipofika mazoezini leo wajue ndiyo wamejiondoa kwenye timu moja kwa moja. Na Hafidh aliwatumia ujumbe wachezaji, lakini nao wakamjibu wanataka na viongozi wawepo leo.
    Leo wachezaji walifika mazoezini kama kawaida, lakini hakukuwa na kiongozi hata mmoja zaidi ya Zahera na wasaidizi wake ambaye alikuwa amekwishajiandaa kwa kuwaita wachezaji wa timu B na baada ya nyota wa kikosi cha kwanza kusistiza mgomo wao Mkongo huyo akaendelea mazoezi na wachezaji wa timu ya vijana watupu.  
    Lakini majira ya Saa 5:15 asubuhi viongozi wakafika, Mashauri, Samuel Lukumay na Hussein Ndama na kufanya mazungumzo yaliyomaliza mgomo huo.  
    Inaelezwa kwamba mgomo huu ni matokeo ya usaili wa wagombea kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa klabu Mei 5, mwaka huu.
    Ikumbukwe viongozi wote wa Yanga walijiuzulu kupisha uchaguzi Mkuu na Baraza la Wadhamini likaunda Kamati ya Usimamizi wa timu hadi uchaguzi utakapofanyika iliyohusisha viongozi waliokuwa madarakani.
    Mwenyekiti wa Kamati ni Lucas Mashauri, Makamu wake, Said Ntimizi na Wajumbe Hussein Ndama, Samuel Lukumay, Hussien Nyika, Moses Katabaro na Maulid Kitenge. 
    Lukumay na Nyika ndiyo walikuwa viongozi wa mwisho kujiuzulu Yanga na walikuwa wakishirikiana na Mashauri, Ntimizi na Ndama kwenye kuongoza timu.
    Mashauri alichukua fomu ya kuwania Uenyekiti, Lukumay Umakamu, Ntimizi na Nyika Ujumbe, lakini wote wakaenguliwa katika usajili kwa sababu mbalimbali.
    Ilichukuliwa kama watu hao waliamua kujivua majukumu ya kuendesha timu baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na sasa mzigo unawaangukia wajumbe wengine, Katabaro na Kitenge ambao hata hivyo hawajawahi kuonekana japo mazoezini tangu wateuliwe.
    Na kinachowaumiza zaidi wachezaji ni kuona zoezi la kuichangia klabu linaendelea vizuri, huku Kocha Zahera akielekeza nguvu zake kwenye kujenga kikosi cha msimu ujao wakati wao wana miezi mitatu hawajalipwa mishahara na wengi wanadai fedha za usajili.
    Wachezaji wanalalamika kwamba hakuna hata usafiri wa kwenda mazoezini na hali zao binafsi ni mbaya kwa sababu hawana mishahara wala posho katika timu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA SC WAKUBALI KUANZA MAZOEZI KESHO BAADA YA MAZUNGUMZO NA UONGOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top