• HABARI MPYA

    Tuesday, April 30, 2019

    BAO LA DAKIKA YA MWISHO LAIPA USHINDI SIMBA SC IKIILAZA JKT TANZANIA PUNGUFU 1-0

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa 1-0 JKT Tanzania Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam jioni ya leo.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 72 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kushika nafasi ya pili, nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga SC wenye pointi 77 za mechi 33.
    Sifa zimuendee mfungaji wa bao hilo pekee dakika ya sita kati ya saba za nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida, kiungo Hassan Dilunga aliyetokea benchi kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Nahodha, John Raphael Bocco.


    Lakini pongezi haswa zimuendee mpishi wa bao hilo, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyewavuruga mabeki wa JKT kwa chenga kabla ya kumpenyezea mpira mfungaji. 
    Na Okwi alipiga bao hilo akitoka kukosa mabao zaidi ya matatu ya wazi kwenye mchezo uliochezeshwa na Heri Sasii aliyesaidiwa na washika vibendera Hellen Mduma na Shaffi Mohammed wote wa Dar es Salaam.
    Nahocha John Bocco aliyefunga mabao yote Simba ikiilaza 2-0 Biashara United mjini Musoma katika mchezo uliopita, leo hakuwa vizuri kiasi cha kupumzishwa baada ya dakika ya 30 tu.
    Na JKT Tanzania inayofundishwa na Kocha Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Mohamed Abdalah 'Bares' ilimaliza pungufu baada ya mchezaji wake, Anuary kilemile kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 74 kufuatia kuonyeshwa njano ya pili kwa kucheza rafu. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly/Nicholas Gyan dk70, Mohammed Hussein, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei/Rashid Juma dk59, Clatous Chama, Muzamil Yassin, John Bocco/Hassan Dilunga dk30, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.
    JKT Tanzania; Abdulrahman Mohammed, Anuary Kilemile, Salim Aziz Gilla/Saad Abubakar dk80, Rahim Juma, Frank Nchimbi, Nurdin Mohamed, Najim Magulu, Mwinyi Kazimoto, Samuel Kamuntu, Edward Songo na Richard Maranya/Kelvin Nashon dk87.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAO LA DAKIKA YA MWISHO LAIPA USHINDI SIMBA SC IKIILAZA JKT TANZANIA PUNGUFU 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top