• HABARI MPYA

    Thursday, April 25, 2019

    WACHEZAJI YANGA WAGOMA HADI WALIPWE MALIMBIKIZO YA MISHAHARA NA FEDHA ZA USAJILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam wamegoma kufanya mazoezi leo asubuhi wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao pamoja na fedha za usajili.
    Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam wakati wachezaji walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.
    Wachezaji wote walifika mazoezini mapema Saa 2:00 asubuhi ya leo, lakini wakawaagiza Manahodha wao, Ibrahim Ajibu na Juma Abdul waende kumuambia kocha Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwamba hawatafanya mazoezi kwa sababu viongozi wamewapuuza.
    Na hiyo ni baada ya jana wachezaji hao kumuomba Zahera ambaye pia ni kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC awaite viongozi kwenye mazoezi ya leo asubuhi ili wajadiliane juu ya stahiki zao.
    Lakini kitendo cha kutotokea kwa kiongozi hata mmoja mazoezini leo kiliwaudhi wachezaji na kukubaliana kuondoka bila kufanya mazoezi.
    Na Kocha Zahera alionyesha msimamo wa kutotaka kujadiliana chochote na wachezaji zaidi ya kuwaamrisha waingie uwanjani kufanya mazoezi. Mwishowe, wachezaji wakaondoka na kocha naye na Maafisa wake wa benchi la Ufundi wakaondoka kinyonge.
    Hayo yanatokea siku nne kabla ya mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Na habari zaidi zinasema kwamba mgomo huu ni matokeo ya usajili wa wagombea kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa klabu Mei 5, mwaka huu.
    Ikumbukwe viongozi wote wa Yanga walijiuzulu kupisha uchaguzi Mkuu na Baraza la Wadhamini likaunda Kamati ya Usimamizi wa timu hadi uchaguzi utakapofanyika iliyohusisha viongozi waliokuwa madarakani.
    Mwenyekiti wa Kamati ni Lucas Mashauri, Makamu wake, Said Ntimizi na Wajumbe Hussein Ndama, Samuel Lukumay, Hussien Nyika, Moses Katabaro na Maulid Kitenge. 
    Lukumay na Nyika ndiyo walikuwa viongozi wa mwisho kujiuzulu Yanga na walikuwa wakishirikiana na Mashauri, Ntimizi na Ndama kwenye kuongoza timu.
    Mashauri alichukua fomu ya kuwania Uenyekiti, Lukumay Umakamu, Ntimizi na Nyika Ujumbe, lakini wote wakaenguliwa katika usajili kwa sababu mbalimbali.
    Inachukuliwa kama watu hao wameamua kujivua majukumu ya kuendesha timu baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na sasa mzigo unawaangukia wajumbe wengine, Katabaro na Kitenge ambao hata hivyo hawajawahi kuonekana japo mazoezini tangu wateuliwe.
    Na kinachowaumiza zaidi wachezaji ni kuona zoezi la kuichangia klabu linaendelea vizuri, huku Kocha Zahera akielekeza nguvu zake kwenye kujenga kikosi cha msimu ujao wakati wao wana miezi mitatu hawajalipwa mishahara na wengi wanadai fedha za usajili.
    Wachezaji wanalalamika kwamba hakuna hata usafiri wa kwenda mazoezini na hali zao binafsi ni mbaya kwa sababu hawana mishahara wala posho katika timu.
    Juhudi za kumpata Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omar Kaaya kuzungumza hali hiyo hazikufanikiwa baada ya simu yake kuwa imezimwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WAGOMA HADI WALIPWE MALIMBIKIZO YA MISHAHARA NA FEDHA ZA USAJILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top