• HABARI MPYA

    Sunday, April 14, 2019

    SAMATTA AFUNGA NA KUSABABISHA BAO KRC GENK IKIICHAPA CLUB BRUGGE 3-1 LIGI YA UBELGIJI

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku huu amesababisha bao la pili na kufunga la tatu kuisaidia timu yake, KRC Genk kuibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Leandro Trossard alifunga bao la kwanza dakika ya 13, kabla ya H. Vanaken kuisawazishia Club Brugge kwa penalti dakika ya 36.
    Mbwana Samatta akapiga shuti likambabatiza beki wa Club Brugge na Ruslan Malinovskiy akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 55.

    Mbwana Samatta amefunga na kusababisha bao KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Club Brugge 

    Ukawadia wakati wa Mbwana kufunga mwenyewe dakika ya 81 , hilo likiwa bao lake la 21 msimu huu na kuihakikishia Genk ushindi wa tatu katika mechi nne za hatua ya pili ya Ligi ya Daraja la Kwanza A Ubelgiji, maarufu kama Championship Round.
    Samatta mwenye umri wa miaka 26, usiku huu amecheza mechi ya 150 kwenye mashindano yote na akiwa amefunga mabao 60 tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

    Mbwana Samatta akishangilia na Leandro Trossard aliyefunga bao la kwanza la Genk

    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 117 sasa na kufunga mabao 45 na kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili na Europa League amecheza mechi 24 na kufunga mabao 14.
    Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Uronen, Lucumi, Dewaest, Maehle, Berge, Heynen/De Norre dk92, Malinovskyi/Wouters dk79, Ito, Trossard/Ndongala dk88 na Samatta.
    Club Brugge: Horvath, Wesley, Diatta, Schrijvers/Openda dk65, Vanaken, Denswil, Vormer, Rits/Amrabat dk45, Dennis/Danjuma dk69, Mechele na Mata.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA NA KUSABABISHA BAO KRC GENK IKIICHAPA CLUB BRUGGE 3-1 LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top