• HABARI MPYA

    Monday, April 29, 2019

    CAMEROON BINGWA AFCON U17 DAR, WAIPIGA GUINEA KWA PENALTI

    TIMU ya Cameroon imetwaa ubingwa wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) 2019 baada ya ushindi wa penalti 5-3 dhidi ya Guinea jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Shujaa wa Cameroon jana alikuwa ni kipa Manfred EKoi aliyeokoa mkwaju wa penalti wa Mohamed Sacko, kabla ya Saidou Moubarak kufunga penalti yao ya mwisho na kuipa timu hiyo taji la pili la michuano hiyo baada ya lile walilotwaa mwaka 2003 nchini Eswatini, wakati huo ikijulikana kama Swaziland. 
    Baada ya dakika 120 ngumu, Steve Mvoue, Nassourou Ndongo, Leonel Wamba, Toni Nang na Moubarak wakafunga penalti za Cameroon wakati Alya Bangoura, Alya Toure na Aboubacar Conte wakafunga za Guinea huku ya Sacko ikiokolewa na Ekoi.

    Ushindi huo ni sawa na Cameroon kuendeleza ubabe kwa Guinea baada ya kuifunga pia 2-0 kwenye mechi ya Kundi B awali. Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad akakabidhi Kombe kwa Nahodha wa Cameroon, Fabrice Ndzie na sherehe zikafuatia Uwanja wa Taifa.
    Mchezaji Bora wa Mashindano ni Steve Mvoue wa Cameroon, mfungaji Bora Osvaldo Capemba wa Angola aliyefunga mabao manne ambaye timu yake nayo imebeba tuzo ya Soka ya Kiungwana.
    Juzi Angola ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika AFCON U17 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Nigeria jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Mabao ya Angola yalifungwa na Osvaldo Capemba dakika ya 28 akimalizia pasi ya David Nzanza na Zito Luvumbo dakika ya  49 akimalizia pasi ya Telson Tome, wakati la Nigeria lilifungwa na Wisdom Ubani dakika ya 30 akimalizia pasi ya Olatomi Olaniyan.
    Ushindi huo ni sawa na kisasi kwa Angola baada ya kufungwa 1-0 na Nigeria katika mchezo wa Kundi A Aprili 17.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAMEROON BINGWA AFCON U17 DAR, WAIPIGA GUINEA KWA PENALTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top