• HABARI MPYA

    Saturday, April 13, 2019

    SAMATTA: SENEGAL NA ALGERIA NI WAKALI LAKINI TUTAKOMAA NAO TUWAONYESHE TUMEDHAMIRIA, KENYA...

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba Senegal na Algeria ni wapinzani wa kiwango cha juu katika kundi lao, lakini watapambana nao kwa dhamira ya kujiinua pia kisoka.
    Tanzania imepangwa Kundi C katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri pamoja na Kenya, Algeria na Senegal.
    Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo kutoka Genk, Ubelgiji, Samatta amesema kwamba Senegal na Algeria ni timu ngumu mno katika kundi lao, lakini watapambana nazo. 

    Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta amesema Senegal na Algeria ni wakali, lakini watapambana nao

    “Hatupo katika kiwango kimoja, kwa maana wao wamekwishapiga hatua katika soka miaka mingi iliyopita, ni lazima tuwaheshimu. Lakini ni lazima tupambane kuwaonyesha kuwa tunakwenda walipo na tuna uchu wa kufika huko,”amesema Samatta.
    Na kuhusu Kenya, Samatta amesema; “Tunawaheshimu majirani zetu wako katika mtiririko mzuri wa maendeleo kisoka, lakini nadhani bado hawajakwenda mbali kutupita,”.
    Mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji amesema kwamba Kundi C ni gumu, kwani linawakutanisha na timu kubwa za Afrika zilizowapita katika viwango kwa kiasi kikubwa, hivyo ni vyema kukawa na maandalizi madhubuti ili kuweza kushindana na pia kujaribu kupenya katika hatua ya mtoano.
    Na mchezaji huyo wa zamani wa klabu za African Lyon, Simba SC za Dar es Salaam na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amesema kwamba Tanzania inatakiwa kujiwekea malengo ya kushiriki kila fainali za AFCON kuanzia sasa.
    Katika droo iliyoongoza na magwiji wa Afrika, Mustapha Hadji wa Morocco, Ahmed Hassan wa Misri, El Hadji Diouf wa Senegal na Yaya Toure wa Ivory Coast usiku wa jana ukumbi wa Sphinx & the Pyramids mjini Giza, wenyeji, Misri wamepangwa Kundi A pamoja na Zimbabwe, Uganda na DRC.
    Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, wakati Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F linazikutanisha Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
    Taifa Stars ilifuzu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    

    Mbwana Samatta ameshauri maandalizi mazuri yafanyike kabla ya AFCON 

    Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
    Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
    Taifa Stars itaanza na Senegal Juni 23 Saa 1:00 usiku, kabla ya kumenyana na Kenya Juni 27 Saa 4:00 usiku Uwanja wa Juni 30 na kumaliza na Algeria Julai 1 Saa 3:00 usiku Uwanja wa Al Salam mjini Cairo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: SENEGAL NA ALGERIA NI WAKALI LAKINI TUTAKOMAA NAO TUWAONYESHE TUMEDHAMIRIA, KENYA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top