• HABARI MPYA

  Thursday, August 16, 2018

  TANZANIA BADO HAISOMEKI FIFA…YABAKI NAFASI YA 140 INAFUATANA NA SUDAN KUSINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imeendelea kuwa miongoni mwa nchi dhoofu kisoka, kufuatia orodha ya viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mwezi Julai kuiacha nafasi yake ya 140.
  Wazi hiyo imechangiwa na timu hiyo kutocheza kwa muda mrefu mchezo wowote – kwani mara ya mwisho Taifa Stars Machi 27, mwaka huu ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.


  Siku hiyo, mabao ya Tanzania yalifungwa na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
  Uganda inayobaki nafasi ya 82 imeendelea kuongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikifuatiwa na Kenya katika nafasi ya 112 na Rwanda nafasi ya 136, wakati Burundi ipo nafasi ya 148 na Sudan Kusini ikiwa nafasi ya 156.
  Mabingwa wa dunia, Ufaransa sasa ndiyo wanashikilia usukani wa soka bora wakifuatiwa na washindi wa tatu katika fainali za Urusi, Ubelgiji ambayo imepanda kwa nafasi moja wakati Brazil imeanguka kwa nafasi moja hadi ya tatu.
  Croatia imepanda hadi nafasi ya nne kutoka ya 16, wakati Uruguay ni ya tano ikifuatiwa na England nafasi ya sita, Ureno nafasi ya saba, Uswisi nafasi ya nane, Hispania ya tisa na Denmark inakamilisha 10 Bora ikiiacha nje Argentina, kwenye nafasi ya 11 baada ya kuporomoka kwa nafasi sita.
  Kwa Afrika, Tunisia ndiyo wanaongoza kwa sasa wakiwa nafasi ya 24 duniani, wakifuatiwa na Senegal, DRC nafasi ya 37, Ghana nafasi ya 45, Morocco nafasi ya 46, Cameroon nafasi ya 47, Nigeria nafasi ya 49, wakati Misri imeangukia nafasi ya 65 kutoka ya 20.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TANZANIA BADO HAISOMEKI FIFA…YABAKI NAFASI YA 140 INAFUATANA NA SUDAN KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top