• HABARI MPYA

  Friday, August 17, 2018

  SIMBA SC WAWASILI MWANZA TAYARI KUIVAA MTIBWA KESHO; KOCHA MBELGIJI ATAMBA WANASHINDA MAPEMA TU

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  KIKOSI cha Simba SC kimewasili mjini Mwanza leo asubuhi tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro Jumapili Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Simba SC inayonolewa na kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems imewasili ikitokea mjini Arusha ambako Jumatano ilicheza mechi ya kirafiki na kushinda 2-1 dhidi ya wenyeji, Arusha United. 
  Akizungumza baada ya kuwasili mjini Mwanza leo, kocha wa Simba SC Aussems amesema kwamba wachezaji wake wote wako vizuri, kasoro Nahodha John Bocco na beki, Shomari Kapombe ambao hawamo kwenye programu ya mchezo wa kesho.

  Aussems amesema kwamba wako vizuri kwa ajili ya mchezo huo na dhamira yao ni kutwaa taji hilo kwa kuwa wanataka kushinda kila taji la michuano wanayoshiriki.
  Mtibwa Sugar nao wanatarajiwa kuwasili leo mjini Mwanza tayari kwa mchezo huo utakaochezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Elly Sasii wa Dar es Salaam, ambaye atasaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Hellen Mduma wa Dar es Salaam, wakati refa wa akiba atakuwa Jeonesya Rukyaa wa Kagera.   
  Simba SC, mabingwa wa Ligi Kuu watakuwa wanacheza mechi ya kuwania Ngao kwa mara ya sita kihistoria, wakati kwa Mtibwa, washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC) watakuwa wanafanya hivyo kwa mara ya pili tu tangu kuanzishwa kwa mchuano huo mwaka 2001.
  Simba SC waliandika historia nyingine katika soka ya Tanzania, baada ya kuwa moja ya timu mbili za kwanza kucheza mechi ya kwanza Ngao mwaka 2001 walipofungwa 2-1 ma mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
  Mchuano huo ukasimama kwa kukosekana mdhamini hadi uliporejea mwaka 2009 na Mtibwa Sugar wakawa mabingwa wa pili baada ya kuwachapa Yanga SC 1-0 Uwanja wa Uhuru.
  Simba SC wakashindwa kutwaa tena Ngao mwaka 2010 baada ya kufungwa kwa penalti 3-1 na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufuatia sare ya 0-0 Uwanja mpya wa Taifa.
  Michuano ya nne ya Ngao ya Jamii mwaka 2011 ndiyo iliipa Simba SC ushindi wa kwanza wa taji hilo, baada ya kuilaza Yanga SC 2-0 Uwanja wa Taifa kabla ya Wekundu hao wa Msimbazi kubeba tena ‘Ubao’ mwaka uliofuata, 2012 baada ya kuifunga Azam FC 3-2.
  Yanga SC wakabeba Ngao ya Jamii mara tatu mfululizo mara zote wakiifunga Azam FC, mwaka 2013 bao 1-0, mwaka 2014 mabao 3-0 na mwaka 2015 kwa penalti 8-7 kufuatia sarte ya 0-0.
  Azam FC wakatwaa Ngao yao pekee ya Jamii mwaka 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 na mwaka jana, Simba SC wakawapiga mahasimu wao wa jadi kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
  Kwa mara ya kwanza kihistoria kesho mechi ya Ngao ya Jamii itafanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam na Mwanza imekuwa na bahati hiyo wakizipokea Simba SC na Mtibwa Sugar kupenua pazia la Ligi Kuu msimu wa 2018-2019. Nani ataibuka mshindi? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAWASILI MWANZA TAYARI KUIVAA MTIBWA KESHO; KOCHA MBELGIJI ATAMBA WANASHINDA MAPEMA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top