• HABARI MPYA

    Saturday, August 11, 2018

    SERENGETI BOYS YAKUTWA NA ‘VIJEBA’ WAWILI…WAENGULIWA MICHUANO YA KUFUZU AFCON 17

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NYOTA wawili wa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Jafary Mtoo na Lenox Fred Chande ni miongoni mwa wachezaji 11 walioondolewa kwenye michuano ya kuwania kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo (AFCON U17) kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
    Wachezaji hao wameondolewa baada ya zoezi la vipimo vya kuthibitisha umri (MRI) zoezi lililofanyika hospitali ya Muhimbili na kusimamiwa na madaktari wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya michuano hiyo ijulikanayo kama CECAFA CAF Afcon qualifier ambayo inaanza leo mjini Dar es Salaam.

    Madaktari wa Hitech Sai Healthcare Centre, Ada Estate, Laila Khan na Baby Khan wakimfanyia vipimo mchezaji wa Serengeti Boys, Ben Anthony Starkie anayechezea Leicester City U16 ya England 

    Wachezaji walioondolewa walikutwa wamezidi umri wa miaka 17 katika vipimo vya madaktari wa CAF iliyobadili mfumo wa mashindano ya kufuzu kwa AFCON U17 ambao ni Yacine Zerquin kutoka Algeria na Sherif Ahmed wa Misri. 
    Taarifa ya Makamu wa Rais wa Kamati ya Tiba ya CAF, Dk Yacine Zerguini imewataja wachezaji wengine walioenguliwa ni Abdoul Intwari wa Burundi, Maxwell Mullili, Lesley Otieno na Abdulmalik Hussein Abdallah wa Kenya, Simon Pitia Alberto wa Sudan Kusini, Gamel Abdou Kamal wa Sudan, Oluka George, Kafumbe Joseph na Elvis Ngonde wa Uganda.
    Michuano ya CECAFA CAF Afcon qualifier inaanza leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kwa mchezo kati ya Rwanda na Sudan Saa 8:00 kabla ya wenyeji, Tanzania kumenyana na Burundi Saa 11:00 jioni na kiingilio ni bure.
    Bingwa wa mashindano atafuzu moja kwa moja kwa AFCON U17 ya mwakani ambayo Tanzania ni mwenyeji.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAKUTWA NA ‘VIJEBA’ WAWILI…WAENGULIWA MICHUANO YA KUFUZU AFCON 17 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top