• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2018

    AMUNIKE KUKUTANA NA MAKOCHA WOTE WA LIGI KUU KUJADILIANA NAO KUHUSU TIMU YA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike atakutana na makocha wote wa klabu za Ligi Kuu kujadiliana juu ya masuala ya kiufundi.
    Hayo yamesemwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online juzi mjini Dar es Salaam.
    Karia amesema kwamba mwalimu anataka kukutana na makocha wa klabu za Ligi Kuu ili kujadiliana nao juu ya masuala ya kiufundi kwa manufaa ya timu ya taifa.
    “Mwalimu atakutana na makocha wote wa timu za Ligi Kuu, lakini pia atakutana na makocha wa timu za taifa na makocha ambao walikwishafundisha timu za taifa, atakuwa na mazungumzo nao ya kiufundi, baada ya hapo tutakaa ataelekeza Kamati ya Ufundi, utaratibu gani ambao upo,” amesema Karia.

    Emmanuel Amunike atakutana na makocha wote wa klabu za Ligi Kuu

    Amunike mwenye umri wa miaka 47, amesaini mkataba wa miaka miwili kufundisha Taifa Stars akichukua nafasi ya kocha mzalendo, Salum Mayanga aliyemaliza mkataba wake Aprili, mwaka huu.
    Taifa Stars inakuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
    Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 amefundisha kalbu za Al Hazm kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 aliporejea nyumbani kufunisha Ocean Boys.
    Alipoachana na U17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.  
    Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
    Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini kabla ya mwaka 2003 kwenda kumalizia soka yake Busan I'Cons alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE KUKUTANA NA MAKOCHA WOTE WA LIGI KUU KUJADILIANA NAO KUHUSU TIMU YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top