• HABARI MPYA

    Saturday, March 17, 2018

    MBIO ZA SIMBA SC MICHUANO YA AFRIKA 2018 ZAISHIA PORT SAID, YATOA SARE 0-0 NA KUTUPWA NJE

    Na Mahmoud Aboud, PORT SAID 
    SAFARI ya Simba SC katika michuano ya Afrika imefikia tamati usiku huu Uwanja wa Port Said baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Al Masry katika mchezo wa marudiano hatua 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Sare huyo inamaanisha Simba SC inatolewa kwa mabao ya ugenini baada sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Machi 7.
    Katika mchezo wa leo, Simba SC iliingia na maarifa ya kucheza kwa kujihami zaidi huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza kupita kwa washambuliaji wake, Nahodha John Bocco na Mganda Emmanuel Okwi.
    Lakini safu ya ulinzi ya Al Masry leo ikiongozwa na beki Muivory Coast, Mohamed Koffi ilisimama imara kudhibiti mashambulizi yote ya Simba.
    Kipa wa Simba SC, Aishi Manula akiwa juu kuokoa moja ya hatari zilizopelekwa langoni mwake leo na  wachezaji wa Al Masry 

    Ahmed Shokry wa Al Masry akimtoka kiungo wa Simba SC, James Koteli leo Port Said

    Al Masry walipata pigo dakika ya 13 baada ya mshambuliaji wao, Farid Emam ‘Shawky’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na nyota wa Burkina Faso mwenye asili ya Ivory Coast, Aristide Bance.
    Mabadiliko hayo kidogo yalipunguza kasi ya mashambulizi ya Al Masry langoni mwa Simba, kwani Bance pamoja na umbo lake kubwa, uwezo wa kumiliki mpira alikuwa hachezi kwa bidii.
    Kipindi cha pili kocha Mfaransa wa Simba, Pierre Lechantre aliamua kuimarisha safu ya ushambuliaji kwa kumtoa beki Yussuf Mlipili na kumuingiza Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 65.
    Lakini Simba nayo ikapata pigo baada ya mabadiliko hayo, kufuatia kiungo Mghana, James Kotei aliyekwenda kucheza nafasi ya Mlipili baada ya kuingia kwa Mavugo kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Shiza Kichuya dakika ya 73.
    Kuanzia dakika ya 80 Al Masry wakaanza rasmi kucheza kwa kujihami, zikiwa ni dakika mbili tu baada ya Mavugo kukosa bao la wazi kwa kupiga shuti lililodakwa na kipa Ahdem Abdelwahab kufuatia pasi ya beki Mghana, Asante Kwasi.
    Simba wakapoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza kati ya tano baada ya kutimia dakika 90 za kawaida.
    Hiyo inakuwa michuano ya pili Simba kutolewa msimu huu, baada ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) na sasa wanarejea nyumbani kuendelea kupambana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Kikosi cha Al Masry kilikuwa; Ahdem Abdelwahab, Ahmed Abdalraof, Mohamed Mahmoud, Ahmed Gomaa, Islam Salem, Amir Mousa, Islam Atta/Abdallah Elshamy dk90+4, Mohamed Emam/Ismal Serry dk85, Farid Shawky/Aristide Bance dk13, Mohamed Koffi na Mohamed Ahmed.
    Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, James Kotei/Shiza Kichuya dk73, Yusufu Mlipili/Laudit Mavugo dk65, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi na John Bocco.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBIO ZA SIMBA SC MICHUANO YA AFRIKA 2018 ZAISHIA PORT SAID, YATOA SARE 0-0 NA KUTUPWA NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top