• HABARI MPYA

    Saturday, March 31, 2018

    NGORONGORO YAJIWEKA PAGUMU KUFUZU AFCON U20 NIGER 2019 BAADA YA SARE YA 0-0 NA DRC LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes imejiweka pagumu katika kinyang’anyiro cha tiketi ya Fainali za vijana wa umri Afrika mwakani nchini Niger baada ya sare ya 0-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa sare hiyo, Ngorongoro inayofundishwa na kocha Ammy Ninje anayesaidiwa na Juma Mgunda, Boniface Pawasa katika mazoezi ya nguvu, Meneja Leopold Mukebezi ‘Tassle’ na kicha wa makipa, Saleh Machuppa italazimika kwenda kushinda ugenini wiki mbili zijazo kwenye mchezo wa marudiano.
    Ngorongoro Heroes haikuwa na bahati tu kwenye mchezo wa leo, kwani ilitengeneza nafasi nzuri za kufunga zaidi ya sita, lakini ugumu ulikuwa kwenye umaliziaji na sana kutokana na umahiri wa safu ya ulinzi ya wachezaji wa DRC wenye miili mikubwa.
    Winga wa Tanzania, Said Mussa ‘Ronaldo’ akienda chini baada ya kuchezewa rafu na beki wa DRC, Katalayi Christian 
    Mshambuliaji wa Tanzania, Paul Peter (kushoto) akikimbilia mpira dhidi ya beki wa DRC, Makangila Beverly 
    Mshambuliaji wa Tanzania, Abdul Suleiman (kushoto)  akienda chini baada ya kusukumwa na beki wa DRC, Mawawu Othnel

    Matumaini ya Ngorongoro Heroes kupata ushindi yalizoroteshwa zaidi na uchezeshaji wa marefa kutoka Uganda, William Oloya aliyepuliza kipyenga akisaidiwa na Dick Okello na Issa Masembe ambao waliruhusu wachezaji wa DRC wenye miili mikubwa kuwachezea rafu vijana wadogo wa Ngorongoro.
    Dakika ya 40 mashabiki walipoga yowe kumzomea refa Oloya baada ya beki wa DRC, Katalayi Christian kumchezea rafu winga, Said Mussa ‘Ronaldo’ nje kidogo ya boksi, lakini hakutoa adhabu yoyote.
    Angalau baada ya hapo, refa huyo kidogo akaanza kuchukua hatua dhidi ya rafu walizokuwa wakichezewa wachezaji wa Tanzania.
    Ngorongoro ilipata pigo dakika ya 60 baada ya kiungo wake mshambuliaji, Said Mussa ‘Ronaldo’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Israel Mwenda.
    Na hapo tayari DRC walikwishaanza kucheza kwa kujihami zaidi kutafuta sare, wakitumia muda mwingi kujiangusha na kuchelewa kuanzisha mipira inapokufa upande wao.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ramadhan Kabwili, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Ally Msengi, Dickson Job, Ali Ng'anzi , Assad Juma, Kelvin Naftal, Paul Peter/Riffat Msuya dk77, Abdul Suleiman na Said Mussa ‘Ronaldo’/Israel Mwenda dk60. 
    DRC; Mobaelwa Salum, Tshimanga Ramazani, Mawawu Othnel, Mangindula Henock, Katalayi Christian, Makangila Beverly, Masikini Baptista, Muleka Jackson, Ngedi Ismael/Kilangalanga Pame dk40, Ifaso Ifunga/Mbombombo dk82 Kande na Pinock Vuvu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGORONGORO YAJIWEKA PAGUMU KUFUZU AFCON U20 NIGER 2019 BAADA YA SARE YA 0-0 NA DRC LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top