• HABARI MPYA

    Thursday, March 22, 2018

    TAIFA STARS YAPUNGUZA UTEJA KWA ALGERIA, YAPIGWA 4-1 TU LEO ALGIERS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepunguza unyonge kwa Algeria, baada ya leo kufungwa mabao 4-1 tu katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, usiku huu.
    Hiyo ni baada ya The Green kuipiga Taifa Stars7-0  Novemba 17, mwaka 2015 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, kipa Ally Mustafa Barthez akifungwa mabao matatu kipindi cha kwanza na kipindi cha pili akaingia Aishi Manula naye akapigwa nne Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida, kiungo Mudathir Yahya akitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 41, baada ya njano ya kwanza dakika ya 22. 
    Siku hiyo, mabao ya Algeria yalifungwa na Yacine Brahimi dakika ya kwanza, Faouzi Ghoulam mawili dakika ya 23 na 59 kwa penalti, Ryad Mahrez dakika ya 43, Islam Slimani mawili moja kwa penalti dakika ya 49 na lingine dakika ya 75 na Carl Medjani dakika ya 72.
    Taifa Stars imepunguza unyonge kwa Algeria leo kufungwa mabao 4-1 kutoka 7-0 mwaka 2015 

    Na leo tena Carl Medjani amefunga moja, wakati mabao mengine yamefungwa na Baghdad Bounedjah mawili na Shomari Kapombe aliyejifunga.
    Baghdad anayechezea Al Sadd ya Qatar alifunga bao la kwanza dakika ya 12akimalizia pasi ya Riyad Mahrez wa Leicester City ya England kabla ya kupsaua katikati ya mabeki wa Taifa Stars Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kudini na Kelvin Yondan wa Yanga Tanzania na kumchambua kipa, Abdulrahman Mohamed wa JKU ya Unguja.
    Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji akapiga shuti zuri dakika ya 14 baada ya pasi ya gardiel Michael Mbaga wa Yanga SC, lakini kipa Faouzi Chaouchi wa MC Alger  ya nyumbani akapangua kabla ya mabeki wake kuondosha kwenye eneo la hatari.
    Zinedine Ferhat wa Le Havre ya Ufaransa alipiga fyongo dakika ya 18 baada ya pasi ya Baghdad ambaye naye alipasiwa na Salim Boukhanchouche wa JS Kabylie ya nyumbani.
    Winga wa Difaa Hassan El – Jadidi ya Morocco, Simon Msuva akaifungia bao la kusawazisha Tanzania dakika ya 20 kwa kichwa cha kuparaza na mpira ukambabatiza Hillel El Arbi Soudani na kumpita kipa Faouzi Chaouchi kufuatia kona ya kiufundi ya winga wa Simba SC ya nyumbani, Shiza Kichuya.
    Dakika moja kuelekea mapumziko, beki wa Simba SC, Shomari Kapombe akajifunga kwa kichwa kuipatia Algeria bao la pili dakika ya 44 akijaribu kuokoa krosi ya Sofiane Hanni.
    Kipindi cha pili Taifa Stars walio chini ya kocha Salum Mayanga wakawa wepesi zaidi na kuruhusu mabao mawili zaidi, kwanza dakika ya 53 Carl Medjani akifunga kwa pasi ya Aissa Mandi kufuatia krosi ya Hillel El Arbi Soudani aliyepokea pasi ya Sofiane Hanni na baadaye Baghdad Bounedjah dakika ya 79 akiwachambua mabeki wote wa Stars na kukamilisha shangwe za mabao za The Green.
    Taifa Stars ilizidiwa katika eneo la kiungo pamoja na kocha Salum Mayanga kupanga watu watatu, Mudathir Yahya wa Azam FC anayecheza kwa mkopo Singida United, zote za nyumbani, Said Ndemla wa Simba na Himid Mao wa Azam FC.
    Baada ya mchezo huo dhidi ya Algeria, Taifa Stars inarejea nyumbani kucheza mchezo mwingine wa kirafiki Jumatatu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kikosi cha Algeria kilikuwa; Faouzi Chaouchi, Carl Medjani, Aissa Mandi, Ramy Bensebaini/ Farouk Chafaï dk68, Sofiane Hanni/Mohamed Lamine Abid dk83, Riyad Mahrez, Zinedine Ferhat, Nabil Bentaleb/Ismael/Bennacer dk60, Salim Boukhanchouche/ Farid El Melali dk89, Hillel El Arbi Soudani/ Mokhtar Benmoussa dk78 na Baghdad Bounedjah.
    Tanzania; Abdulrahman Mohamed, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Said Ndemla/Erasto Nyoni dk62, Himid Mao, Mbwana Samatta, Simon Msuva/Rashid Mandawa dk89 na Shiza Kichuya/Mohammed Issa ‘Banka’ dk74.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAPUNGUZA UTEJA KWA ALGERIA, YAPIGWA 4-1 TU LEO ALGIERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top