• HABARI MPYA

    Monday, March 26, 2018

    MBONDE, NIYONZIMA WAANZA KUJIFUA RASMI SIMBA SC, KOCHA MFARANSA NAYE AREJEA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI majeruhi wa muda mrefu Simba SC, beki mzawa Salim Mbonde na kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima wamefanya mazoezi leo kuelekea mechi na Njombe Mji FC Aprili 3.
    Simba SC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Aprili 3, mwaka huu Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kuelekea mechi hiyo Mbonde na Niyonzima wameleta tumaini jipya kikosini.
    Niyonzima yuko mazoezini kwa siku ya tatu leo Simba SC baada ya kurejea kufanyiwa upasuaji nchini India, wakati Mbonde ndiyo ameanza rasmi mazoezi leo.
    Haruna Niyonzima (kulia) na Salim Mbonde (kushoto) wakiwa mazoezi Uwanja wa Boko Veterani leo mjini Dar es Salaam
    Nahodha, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyeumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Al Masry wiki iliyopita naye pia leo amefanya mazoezi.
    Simba ilitoa sare ya 0-0 na Al Masry Machi 17 na kutolewa kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya 2-2 Machi 7, mwaka huu kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
    Na baada ya kutolewa kwenye michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Novemba mwaka jana wakifungwa na Green Warriors ya Mwenge kwa penalti baada ya sare ya 1-1, Simba SC wana nafasi moja tu kucheza michuano ya Afrika mwakani, ambayo ni kupitia Ligi Kuu ambako bingwa wake hucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. 
    Na bahati nzuri kwao, Simba SC ndiyo wanaoongoza Ligi Kuu kwa wastani wao mzuri wa mabao baada ya kulingana kwa pointi na mabingwa watetezi, Yanga SC 46 kila timu, ingawa pia Wekundu wa Msimbazi wana mechi moja mkononi.   
    Wakati huo huo: Kocha Mfaransa wa Simba SC, Pierre Lechantre aliyekuwa nyumbani kwao kwa mapumziko, amerejea jana na leo alikuwepo mazoezini Uwanja wa Boko Veterani kuiandaa timu kwa mchezo dhidi ya Njombe Mji FC Aprili 3.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBONDE, NIYONZIMA WAANZA KUJIFUA RASMI SIMBA SC, KOCHA MFARANSA NAYE AREJEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top