• HABARI MPYA

    Sunday, March 18, 2018

    KARIA, WAMBURA WANAIPELEKA WAPI TFF, SOKA YA TANZANIA?

    TASWIRA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imezidi kuharibika baada ya mgogoro uliobuka baina ya viongozi wa shirikisho hilo, uliosababisha hadi Makamu wa Rais, Michale Richard Wambura kufungiwa maisha.
    Kamati ya Maadili ya TFF imemfungia maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Wambura amefikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
    Kwa upande wake, akizungumzia hatua hiyo, Wambura alisema kwamba Kamati iliyomfungia haina mamlaka, kwa sababu yeye anawajibika kwenye Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu, kwa sababu yeye anawajibika kwenye kamati ya utendaji na Mkutano Mkuu.
    Wambura pia alisema suala la kujilipa fedha kupitia, JECK SYSTEM LIMITED ni suala la muda mrefu sana na lipo chini ya TAKUKURU na akadai kwamba jambo hilo limepangwa kimikakati na sio suala la kisheria, kwani hapo kuna mambo matatu, ajira za TFF, Fedha na Makamu.
    Wambura akasema katika suala la ajira ni baada ya kuleta hoja juu ya nafasi ya Katibu Mkuu kuhitaji wa kuajiriwa na kwamba kwa nafasi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Fedha, alibaini mambo mengi juu ya matumizi mabaya ya fedha na ndivyo vimemjengea chuki kwa wenzake.
    Na tangu juzi kumekuwa na taarifa za Wambura kuwa katika mpango wa kukata Rufaa, lakini inaelezwa kwamba kila alipokwenda amekuwa akikuta ofisi za TFF zimefungwa kiasi cha kuamua kuwasilisha rufaa yake kwa njia ya EMS ili awe ndani ya muda.
    Inawezekana tuhuma za Wambura zikawa na ukweli ndani yake, lakini namna suala hili lilivyoibuliwa na kupelekwa haraka haraka linatia shaka na kubadili mwelekeo kutoka hatua hadi mapambano baina ya wao kwa wao ndani ya TFF.
    Ni Agosti tu mwaka jana umefanyika uchaguzi wa TFF mjini Dodoma na Wambura akiwa mgombea wa kutoka nje ya uongozi alipitishwa na akaenda kushinda – hivyo hatua hizi kuchukuliwa hata uongozi mpya chini ya Rais Wallace Karia haujatimiza mwaka mmoja inafikirisha mno. Kuna nini zaidi? 
    Lakini kikubwa ni namna mambo yanayofanyika katika hali ambayo huwezi kusita kusema ni kwa kukomoana, wakati yangeweza kufanywa katika misingi na taratibu nzuri hata watu wanaofuatilia sakata lenyewe wakaafiki.
    Dhahiri hii inachafua taswira ya TFF, ambayo imekwishaanza kuharibika tangu mwaka jana, kufuatia aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi pamoja na Katibu wake, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga kuswekwa rumande tangu Julai mwaka jana kwa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha.
    Tulitarajia umakini wa hali ya juu kipindi hiki kutoka kwa uongozi mpya, ambao kwa hakika Serikali ilikwishajenga imani na matumaini makubwa juu yao – lakini bahari mbaya inakuwa tofauti.
    Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba haya yanatokea muda mfupi mno tangu Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino azuru Tanzania akiongozana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Ahmad ambao kwa pamoja walikutana hadi na Waziri Mkuu wa nchi, Dk. Kassim Majaliwa. Inasikitisha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA, WAMBURA WANAIPELEKA WAPI TFF, SOKA YA TANZANIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top